SUAMEDIA

Masalia ya Mazao kutumika kutengeneza Shamba la kuoteshea Uyoga

Imeelezwa kuwa masalia ya mazao mbalimbali kama vile Mahindi, mabua ya Mpunga, Karanga, Maharage au Magunzi yanaweza kutumika kwa ajili ya kutengeneza Shamba la kuoteshea Uyoga.

                                

Ameeleza hayo Bw. James Mnhonya Mtaalam wa Maabara kutoka Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi, Idara ya Sayansi ya Viumbe (Biasciancies) katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wakati akizungumza na SUAMEDIA Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki mjini Morogoro.

Amesema ili mtu aweze kutengeneza Shamba la Uyoga vitu vinavyohitajika ni Mbegu, vimengenywa ambavyo vinaweza kuwa masalia ya mazao yoyote yale mfano masalia ya Mpunga ambapo kitu cha kufanya ni kuyaloweka kwenye maji na hatua nyingine ni kuyachemsha ili kuua vimelea vyote.

Vile vile baada ya maji hayo kuchemshwa yanaachwa yapoe kisha zinachukuliwa Mbegu kwa ajili ya kupanda kwenye vifungashio huku unaweka majani na kuendelea kusia mbegu ambapo mfuko ukishajaa unafungwa na kamba na hapo shamba lako litakuwa tayari, hatua inayofuata ni kutoboa matundu machache kwenye kifungashio ili kuruhusu hewa hivyo shamba litakuwa tayari.

Shamba hilo kinatakiwa kuhifadhiwa sehemu ya giza na kama hakuna giza unaweza kutumia mfano wa dumu ambalo ni jeusi hilo litatoa giza la kutosha, unaweka hapo kwa majuma mawili alafu utaona jinsi Uyoga unavyotamalaki kwenye vile vimengenywa, ameeleza Bw. Mnhonya

Baada ya majuma mawili unatoa unaweka mahali penye mwanga lakini penye unyevu wa kutosha alafu baada ya majuma mengine mawili au matatu utaona uyoga unaanza kuchipua, unakomaa na kuwa tayari kuliwa au kuuzwa, ameeleza zaidi.

Aidha Bw. Mnhonya amesema masalia yanayobaki baada ya kuvuna Uyoga yanaweza kutumika kulishia Wanyama na kurutubishia bustani kwa maana ya Ardhi unayotumia kwa ajili ya Kilimo.

Aidha Mtaalam huyo ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro na Maeneo ya jirani kufika banda la SUA kwenye Maonesho hayo ya Nanenane kwa ajili ya kujionea kwa macho lakini pia kujifunza kulima Uyoga ambao ni lishe bora, dawa na tiba  kwa binadamu na Wanyama vilevile ni fursa nzuri ya kujiongezea kipato.





Post a Comment

0 Comments