SUAMEDIA

Wananchi waaswa kutumia dawa za asili

 

Na: Farida Mkongwe

Watanzania wametakiwa kutumia zaidi dawa za asili zinazotokana na miti dawa ambazo zimethibitishwa na Shirika la Viwango Nchini (TBS) kwa sababu dawa hizo za asili hutumika kama chakula tofauti na dawa nyingine ambazo ukizitumia kwa muda mrefu zinatengeneza usugu mwilini na hivyo hata ukiugua inakuwa ni vigumu kupona kwa kutumia dawa hizo.



Fundi Maabara kutoka Idara ya Kemia na Fizikia katika Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Bi. Aneth Coster akiwa na dawa asili kwenye banda la SUA. Picha na Asifiwe Mbembela.

Wito huo umetolewa Julai 20, 2023 na Fundi Maabara kutoka Idara ya Kemia na Fizikia katika Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Bi. Aneth Coster wakati akizungumza na SUAMEDIA katika viwanja vya Maonesho ya Vyuo Vikuu yanayofanyika Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam kuhusu dawa za asili zinazotengenezwa na Idara hiyo.

Bi. Aneth amezitaja dawa zilizopo katika maonesho hayo kuwa ni Synadol ambayo inatibu mafua makali, kifua, pumu na mafindofindo ambayo imetengenezwa kwa kutumia mti dawa baada ya kufanyiwa tafiti za kutosha na kubaini mti huo una uwezo wa kutibu magonjwa hayo.

“Pia tuna dawa nyingine inayotibu ngozi ambayo ipo katika mfumo wa sabuni na imetengenezwa kwa kutumia mti dawa unaoitwa Mvunja kongwa ambao kitaalamu unalikana kwa jina la Synadenium na majani yake nayo yamefanyiwa tafiti na kuona yanatibu kwa hiyo sabuni hizi zimetengenezwa kwa kutumia majani na mizizi na zinatibu ngozi kama imeathirika na fangasi”, amesema Bi. Aneth.

Dawa nyingine ambazo zimetengenezwa na Idara hiyo ya Kemia na Fizikia ni dawa ya kusafisha na kungarishia sinki la chooni hasa likiwa na uchafu korofi, pamoja na vitasa mikono (sanitizer).

“Tafiti zinaendelea na pia tuna kitu kinaitwa indicator (viashiria) hivi vinatumika kwenye kuweza kuchanganya tindikali mbili base na acid ili upate neutralization yaani upate end point kwa hiyo tuna indicator ile ambayo imetengenzwa kwa miti nia yetu kubwa ni kwamba badala ya kuendelea kutumia indicator ambazo tunazinunua toka nje tufike mahala tutumie bidhaa zetu za ndani ili kupunguza gharama”, amesema Bi. Aneth.

Baadhi ya dawa, sabuni na vitakasa mikono vinavyotokana na miti ya asili. Picha na Asifiwe Mbembela


Post a Comment

0 Comments