SUAMEDIA

SUA yajidhatiti kutoa elimu bora

 

Na Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesema kitaendelea kuwa Chuo bora nchini kwa kutoa tafiti zenye matokeo chanya kwa jamii sambamba na kuendelea kufundisha Program mbalimbali zinazofanyika kivitendo zaidi kwa lengo la kutoa wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kuajirika.

Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda (kushoto) akitoa maelezo kwa Mtafiti Mwandamizi Dkt. Devotha Mosha wakiwa kwenye banda la SUA

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akizungumza kwenye banda la Chuo hicho katika Maonesho ya Vyuo Vikuu yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam.

Prof. Chibunda ametoa rai kwa wazazi na wanafunzi kufanya maombi ya kujiunga na SUA kwa sababu Chuo hicho kina kozi mbalimbali ambazo zimewanufaisha wahitimu wengi nchini ambao wamekuwa msaada kwa jamii na kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Natumia nafasi hii kuwakaribisha waombaji wote wanaotaka kujiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, ukitaka kusoma na baadaye usitembee na bahasha ya kutafuta kazi ili wewe uwe umejengwa kwenda kujipatia kazi lakini hata utakapoajiriwa uweze kuwa ni mfanyakazi mwenye ufanisi chuo cha kuja kusoma ni SUA”, amesema Prof. Chibunda.

Amesema kuwa mwitikio wa wanafunzi kujiunga na Chuo cha SUA ni mkubwa kwani kwa siku mbili tu wanafunzi karibu 4,000 wamejitokeza kufanya maombi ya kujiunga na Chuo hicho.

“Kwa hiyo nitumie hii nafasi kuwaomba wazazi lakini pamoja na waombaji waingie kwenye tovuti ya Chuo chetu waangalie kozi ambazo tunazitoa lakini waangalie na mbinu za ufundishaji wetu, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ni Chuo mahususi cha kipekee kwa ajili ya kuandaa vijana wa  nchi hii ili baadaye wakawe wenye tija katika nchi yetu”, amesema Prof. Chibunda.

Maonesho ya Vyuo Vikuu nchini ambayo yalifunguliwa rasmi na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda yalianza Julai 17, 2023 na yatahitimishwa Julai 22 mwaka huu.




Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda

 (aliyevaa suti ) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa SUA ambao wanashiriki katika Maonesho ya VyuoVikuu

Post a Comment

0 Comments