SUAMEDIA

SUA yaanzisha mashirikiano na Chuo Kikuu CCS Haryana nchini India


Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanzisha mashirikiano na Chuo Kikuu cha Chaudhary Charan Singh Haryana cha Kilimo Hisar (CCSHAU) ili kuimarisha shughuli za utafiti, kubadilishana wanataaluma na wanafunzi na kuanzisha mafunzo ya pamoja kati ya taasisi hizi. Hafla ya uzinduzi wa mashirikiano hayo ilifanyika katika viwanja vya Maonesho vya Sabasaba jijini Dar es Salaam siku ya Jumanne tarehe 11 Julai 2023.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rasi wa Ndaki ya Kilimo kutoka SUA, Profesa Bernard Chove ambaye alimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo wa SUA alisema “Tumejipanga vema kuona Vyuo vyetu vya SUA na CCSHAU vinaendeleza mahusiano ya kuinua taaluma, tafiti na ugani ili kuhakikisha Elimu ya Juu inakuwa chachu ya maendeleo nchini Tanzania na India”.


Kwa upande wa Chuo Kikuu cha CCS Haryana cha Kilimo, Makamu wa Mkuu wa chuo hicho, Profesa Baldev R. Kamboj alisema “Leo ni siku ya furaha kwangu na wanajumuiya wa CCSHAU kushuhudia kuanzishwa kwa mashirikiano kati ya Vyuo vyetu, makubaliano yetu yasiishie kusaini makaratasi bali tuyaweke katika utekelezaji mapema kadri iwezekanavyo”. Prof. Kamoj alisisitiza.


Katika kuhakikisha utekelezaji wa mashirikiano unaanza mara moja, Chuo Kikuu cha SUA kitapokea wanataaluma wa fani ya Uhandisi wa Kilimo ili kuja kushirikiana na wenzao wa SUA katika kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa SUA. Pia vyuo vikuu hivi vimekubaliana kufanya juhudi katika kuanzisha Kituo cha Pamoja cha Atamizi na Teknolojia nchini Tanzania ili kuhakikisha wanafunzi wa Tanzania na India wanapata mafunzo kwa vitendo na hivyo kuwaandaa kikamilifu katika upatikanaji wa ajira baada ya mafunzo yao. Aidha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo hivi karibuni kinatarajia kutuma timu ya Menejimenti nchini India kutembelea na kujifunza zaidi kutoka kwa wenzao wa CCSHAU na kubainisha maeneo zaidi ya mashiriano katika kutekeleza makubaliano yao.

 

C:\Users\User\Pictures\Screenshots\Screenshot (54).png

Profesa Bernard Chove na Profesa Baldev Kamboj wakisaini Hati ya Mashirikiano kati ya SUA na CCSHAU jijini Dar es Salaam




C:\Users\User\Pictures\Screenshots\Screenshot (55).png

Prof. Bernard E. Chove akibadilishana Hati ya Mashirikiano na Makamu wa Mkuu wa Chuo cha CCS Haryana, Profesa Baldev R. Kamboj



Post a Comment

0 Comments