SUAMEDIA

SUA waendelea kuyaishi maono ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Nyerere.

Na: Calvin Gwabara - Morogoro.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Othman Chande amesema ushirikiano Mkubwa uliopo kati ya Baraza lake, Wanafunzi, Wanataaluma na wanajumuiya wote ndio unaosababisha Chuo kusimamia misingi aliyoiweka baba wa Taifa Mwl. Nyerere.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Othman Chande akifuatilia sherehe za mahafali SUA.


Mhe. Chande ameyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari waliotaka kujua mchango wa Chuo hicho kwenye maendeleo ya Kilimo nchini na namna Baraza hilo linavyosimamia kauli ya Baba wa Taifa ya kutoa Elimu kwa vitendo

“Katika Chuo chetu tunaushirikiano mkubwa sana katika utekelezaji wa majukumu yetu kati ya Baraza na Menejimenti ya Chuo, Wanataaluma, Watumishi waendeshaji na Wanafunzi na ushirikishwaji ni mkubwa ndio maana hata wanafunzi wanapata muwakilishi kwenye kikao kikubwa cha Chuo ambacho ni Baraza ambalo ndio chombo kinachotoa Sera na Miongozo ambayo inatekelezwa na Menejimenti” alieleza Jaji Chande.

Amesema mkazo mkubwa wa SUA sio tuu kutoa cheti bali kutoa wahitimu wenye sifa na uwezo wa kuingia kwenye ushindani katika soko la ajira, kujiajiri lakini pia kutoa ajira kwa wengine na kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia Kilimo na sayansi zingine zinazoendana na hizo.

Aidha Mhe. Chande amesema ubora wa wahitimu wa Chuo hicho unatokana na kuwa na Wahadhiri waliobobea hali ambayo imedhihirishwa kwa miaka kadhaaa watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kuongoza kwa machapisho yao Tanzania na kufanikiwa kutoa watafiti bora Tanzania na Afrika tafiti ambazo mchango wake si kwa Tanzania pekee bali Afrika na Dunia.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Chuo amesema kwa miaka kadhaa Chuo kimefanya tafiti mbalimbali ambazo matokeo yake na watafiti wake wamechangia katika kutengeneza na kuboresha Sera na kutoa Ushauri kwa Taifa katika Kilimo, Mifugo, Mazingira, Afya na Elimu.

Ametumia nafasi hiyo kuishurkuru Serikali kwa kuwezesha kupata kiasi cha shilingi Bilioni 73 kupitia mradi wa HEET fedha ambazo zinakwenda kuleta mageuzi makubwa na ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji kwa kuongeza majengo na kununua vifaa vya kisasa ikiwemo kutilia mkazo matumizi ya TEHAMA Chuoni.

“ Sisi kama Chuo kupitia Misitu yetu ya Mafunzo ya Olmotonyi, Mazumbai na Madaba inasaidia kufundishia Wanafunzi na kufundisha jamii namna bora za kupanda miti, kutunza  misitu na kuivuna kwa njia endelevu na kujipatia kipato hivyo mradi wa HEET pia utagusa kwenye kupanua msitu wetu wa kupanda Songea na itasaidia kuongeza mapato ya Chuo chetu” alieleza Mhe. Jaji Chande.

Amesema Chuo kimeendelea kuongeza mapato ya ndani na hivyo kusadia kutatua changamoto mbalimbali zinazokikabili na kufikia kuingiza mapato ya zaidi ya asilimia 25% lakini bado wanaendelea kubuni miradi na mbinu zingine mbalimbali ambazo zitaongeza mapato ya chuo zaidi kila mwaka.

Mwenyekiti huyo wa Baraza pia amesema moja ya mikakati ya Bazara na Chuo ni kuhakikisha wanaongeza udahili wa wanafunzi katika kozi zote kila mwaka kutoka wanafunzi 6,000 kwa Mwaka hadi kufikia 10,000 na hivyo kuruhusu Watanzania wengi zaidi kupata elimu bora katika Chuo hicho cha kipekee cha Kilimo Tanzania.




  

Post a Comment

0 Comments