SUAMEDIA

SUA ni Chuo salama kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu

 Na Josephine Mallango 

Imeelezwa kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ni Chuo salama kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa ulemavu unaoonekana na usioonekana.

Hayo yamesemwa na wadau wa Elimu kutoka SUA Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi wakati wa mafunzo ya utambuzi wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu yaliyotolewa kwa walimu , waendeshaji na wanafunzi wa Kampasi hiyo kwa ufadhili wa mradi wa HEET.

Mratibu wa Mahitaji Maalum kupitia Mradi wa HEET kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Dkt. Thabita Lupeja akifungua mafunzo hayo amesema miongoni mwa vipaumbele katika mradi wa HEET ni kuwatambua wanafunzi wa Vyuo vikuu wenye mahitaji maalum na kuwawezesha katika kuhakikisha wanafunzi hao wanatimiza malengo yao ya kielimu bila vikwazo.

"Wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa ulemavu unaooneka na usioonekana wanahitaji kuona SUA ni sehemu salama ya kuishi pamoja na kujifunza kwa kupata Elimu sawa na wanafunzi wengine na siyo kunyanyapaliwa na kutengwa", amesema  Dkt. Lupeja.

Ameongeza kuwa baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo wa HEET kwa kupata fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia wamekuta kulikuwa na uhitaji mkubwa katika nyanja hiyo ya mahitaji maalumu ambapo mpaka Sasa zaidi ya wanafunzi 258 katika kampasi 2 wamegundulika kuwa wana mahitaji maalumu tofauti kwa ulemavu unaooneka na wengine usiooneka baada ya vipimo mbalimbali vinavyooambatana na mafunzo ambavyo vipimo hivyo utolewa na watalaamu wa Elimu kutoka maeneo mbalimbali wanaoshirikiana na SUA katika kutekelezaji wa mradi huu.

" Bado tunaendelea kuwabaini wanafunzi wenye mahitaji maalumu ikiwemo wenye uono hafifu , changamoto ya uziwi, kutosikia vizuri na nyingine walizozipata Sasa au awali walikuwa nazo na hawakuweka wazi  ili wahitaji waweze kupata hafua stahiki katika kuhakikisha wanamaliza masomo yao wakiwa wanafunzi bora pasipo vikwazo vya kutengwa wala kunyanyapaliwa na kwenye soko la ajira kujiajiri au kuajiriwa wakawe bora", amesema Dkt. Lupeja.

Mratibu huyo ametoa wito kwa wanafunzi wanaojiunga na Chuo cha SUA kuwa wawazi ili waweze kuwezeshwa na kusaidiwa katika kuhakikisha wanajifunza vizuri na kupata huduma inayozingatia mahitaji husika ili wasome na kupata Elimu sawa na wengine. 

"Kuna athari katika kuficha changamoto kuna mfano hai wa mwanafunzi mmoja alificha changamoto yake akaishia kushindwa kuendelea na Chuo akashindwa kuendelea na hiyo ina maana alijisababishia masomo yamuweke pembeni kwa kuwa hakuweza kuwezeshwa kupata huduma stahiki  kwa kujificha kwake mwenyewe lakini baadae akakata rufaa akagundulika ni muhitaji kweli akapewa fursa na sasa anaendelea na masomo lakini hatutakiwi kufika huko muhimu ni  kuelezea changamoto mapema kutatoa mazingira wezeshi ya kujifunza na kufaulu", amefafanua Dkt. Lupeja.

Kwa upande wake mwezeshaji wa masuala jumuishi ya utambuzi  wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu  kutoka Chuo Kishiriki cha Elimu Dar-es-salaam( DUCE) Mkuu wa Kitengo Cha Elimu Maalumu Benigno Kumpanga amesema changamoto iliyopo ni wanafunzi wengi wao wanapojiunga chuoni kwa Mara ya kwanza wanaficha changamoto zao kwa sababu mbalimbali wanazofahamu na kwamba ndio maana miongoni mwa mafunzo hayo ni mbinu zipi zitumike katika kuwatambua wenye mahitaji maalum ikiwemo kama kuna taarifa za walipotoka katika shule zao za  sekondari , taarifa ya kitabibu au kwa kuona baadhi ya matendo yatakayochochea Ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi kuwapeleka wanafunzi wahitaji katika vituo vya afya vya Chuo ili kuwabaini na kuwawezesha kupata mazingira rafiki katika masomo yao kwa kuwa ni haki ya kimsingi.

Naye Mwezeshaji Mratibu kutoka kitengo Cha Elimu Jumuishi AMUCTA (Saut-Tabora ) Fraterinus Osward ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usikivu amesema Mitazamo ambayo bado ipo kwa jamii yenye dhana ya kuwaona watu wenye ulemavu Kama kikwazo ni miongoni mwa unyanyapaa uanaotakiwa kuisha kabisa kwa kuendelea kutoa Elimu .

" Ipo pia dhana  ya kwamba watu wenye mahitaji maalumu wanatakiwa kusoma education pekee siyo kwenda kwenye vyuo vyenye fani nyingine hiyo nayo ni kikwazo kinachochangia wanaojiunga na vyuo vikuu vingine hasa wenye ulemavu usioonekana kuficha changamoto zao  kwa kuhofia kuonekana tatizo na wanaweza kupoteza sifa ya kuwepo chuoni jambo ambalo si la kweli kwa kuwa katika fomu za kujiunga kuna vipengere na ukivijaza unapata uwezeshaji wa mahitaji maalumu kutokana na aina ya uhitaji wako".

Osward ameongeza kuwa watu wenye ulemavu wako sawa na wengine wanachohitaji ni mazingira wezeshi yatakayo waondolea vikwazo ili wafanye kazi na kujiingizia kipato hivyo hawastahili kunyimwa Elimu kwa kuwa kumnyima Elimu kwa dhana potofu ni kumzalishia changamoto ya utegemezi kwenye maisha yake ya baadae lakini ukimuwezesha na kumpa Elimu anajitegemea mwenyewe kwa kujiingizia kipato cha kila siku.

Kwa upande wake Kaimu Mshauri wa Wanafunzi kutoka Kampasi ya Edward Moringe SUA Hilda Gamuya amesema Chuo kimekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanapata stahiki zao ambao wameweka wazi changamoto zao na ambao wanazipatia chuoni hapo ambapo kuna wakati walitumia viongozi wa madarasa kubainisha changamoto hizo kwa wanafunzi wenzao katika madarasa yao Jambo ambalo lilifanikiwa na kwamba bado wanaendelea kwa kuwa hilo ni zoezi endelevu maana mwanafunzi anaweza pata changamoto hata akiwa ameanza masomo au katikakti ya masomo na hivyo kuhitaji kuwezeshwa ili kusoma katika mazingira stahiki .

"Chuo kilishaanza kuwa na miundombinu rafiki na mazingira wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kwamba mradi wa HEET umekuwa  na muendelezo kwa upana wake hivyo wanafunzi wanapswa kujitokeza bila huoga kuweka wazi changamoto zao ili zitatuliwe kwa wakati zisigeuke kikwazo cha kujipatia Elimu".

Naye Rasi wa Ndaki Kampasi ya Mizengo Pinda Prof. Josiah  Katani amesema wanafunzi wanaojiunga SUA Ndaki ya Katavi wajiunge na uhakika wa mazingira wezeshi na salama ya kujifunzia kwa kuwa tayari  wameshachukua hatua na kuweka  miongozo kwa kupitia mafunzo hayo. 












Post a Comment

0 Comments