SUAMEDIA

Panya Buku wa SUA kudhibiti Utoroshaji wa nyara za Serikali

 

Na: Farida Mkongwe

Katika kuhakikisha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinashirikiana na Serikali kutokomeza utoroshaji wa nyara za serikali, Chuo hicho kimeendelea na Mradi wa utafiti wa kuwafundisha Panya buku kuweza kunusa nyara zinazotokana na wanyamapori ambapo utafiti huo umeonesha matokeo chanya.

Msimamizi wa Tafiti kutoka Mradi wa Apopo SUA Bw. Said Mshana akiwa kwenye banda la SUA  akizungumzia Mradi Apopo kuhusiana na utafiti wa Panya buku. Picha na Asifiwe Mbembela.

Msimamizi wa Tafiti kutoka Mradi wa Apopo SUA Bw. Said Mshana ameeleza hayo wakati akizungumza na SUAMEDIA Julai 20,2023 kwenye Maonesho ya Vyuo Vikuu yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam.

Mshana amesema Serikali imekuwa ikitumia nguvu nyingi kuhakikisha kuwa nyara za wanyamapori hazitoroshwi kwenda nje ya nchi na kwamba Mradi huo unashirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori  Tanzanai (TAWA) kuendelea kuwafundisha Panya buku kufanya utambuzi wa nyara hizo ambazo hazitakiwi kusafirishwa nje ya nchi.

Msimamizi huyo wa Tafiti amezitaja tafiti nyingine ambazo zimefanywa kwa mafanikio kwa kutumia panya buku kuwa ni pamoja na utafiti wa kuwafundisha panya buku kufanya utambuzi wa kunusa na kuonesha sehemu ambazo yamefukiwa mabomu ya ardhini.

“Mbali na upande wa mabomu ya ardhini lakini Panya hawa hawa tumewafundisha kunusa vimelea vya kifua kikuu na hivyo tukishirikiana na wenzetu wa Wizara ya Afya pamoja na hospitali ambazo tunashirikiana nazo tumekuwa ni msaada mkubwa sana wa kuweza kuwagundua wagonjwa wa kifua kikuu mapema na kuweza kupata matibabu mapema”, amesema  Mshana.

Ameongeza kuwa bado kuna tafiti mbalimbali zinaendelea kufanyika moja wapo ikiwa ni kuwafundisha Panya kutafuta watu waliokwama kwenye majengo yaliyobomoka ama kufukiwa na vifusi vikubwa.

Amesema Panya hao  wanasaidiwa na vifaa maalum ambavyo wanavibeba mgongoni vikiwa na kamera na vinasa sauti ambavyo vinasaidia waokoaji kuona hali halisi ya ndani ambako panya wameingia kwa ajili ya kuwafuta wahanga na kurusha taarifa au kupata picha za ndani na hivyo kuweza kuelekeza nguvu eneo ambalo watu wamekwama.

Kwa upande wa panya, wagunduzi wa kifua kikuu tunafanya kazi na kliniki na hospital zaidi ya 80 kwa Tanzania ndani ya mikoa minne ikiwepo mkoa wa Morogoro, Dar Es Salaam, Pwani na Dodoma na mpaka sasa panya hawa wameweza kutambua zaidi ya wagonjwa 22, 000 ambapo kwa upande wa nje ya nchi panya hawa wanafanya kazi katika nchi ya Ethiopia na Msumbiji”, amesema Mshana.

Mshana amesema kuhusu panya ambao wanafanya kazi ya kutambua mabomu ya kuzika ardhini kwa sasa wanafanya kazi katika nchi nne ambazo ni Msumbiji, Angola, Cambodia na nchi ya Azerbaijan na toka waanze kazi hiyo ya utambuzi wa mabomu wameshasafisha mita za mraba zaidi ya milioni 70 na kuzirudisha kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Post a Comment

0 Comments