SUAMEDIA

Watafiti wachanga SUA hakikisheni mnarithi mbinu bora za kufanya utafiti - Prof. Sanga

Na Gerald Lwomile

Watafiti wachanga kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kuhakikisha wanarithi ubora wa watafiti nguli ambao muda wao umemalizika ama kwa kustaafu au kutokuwepo SUA ili kuhakikisha chuo kinaendelea kuwa nambo moja katika kufanya utafiti nchini na kusaidia taifa katika mambo ya maendeleo.

Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Utawala, Fedha na Mipango Prof. Camilius Sanga akifunga warsha ya siku 3 ya watafiti wachanga SUA (Picha zote na Gerald Lwomile)

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Utawala, Fedha na Mipango Prof. Camilius Sanga wakati akifunga warsha ya siku 3 iliyoandaliwa kwa watafiti wachanga ambao wamepata fursa ya kujifunza namna bora zaidi za kufanya utafiti, kuandika miradi ya kitafiti, kutafuta wafadhili wa miradi  na namna bora ya kusimamia miradi hiyo ili ilete tija.

Prof. Sanga amesema chuo kitaendelea kuhakikisha kinatoa ushirikiano wa kutosha kwa watafiti hao ikiwa ni pamoja na rasilimali mbalimbali kama vile vitendea kazi na fedha ili kuhakikisha wanafikia malengo yao.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufunga warsha hiyo ya mafuzo, Mratibu wa mafunzo ambaye pia ni  Mratibu wa Utafiti na Machapisho SUA Prof Japhet Kashaigili  amesema wao kupitia Programu ya kuwasaidia watafiti wachanga ya SUARIS  kinaona mwanga wa kuwepo kwa watafiti bora zaidi miaka ijayo kwani watafiti hao wanaonekana kuzingatia mafunzo lakini pia wana kiu ya kufanya tafiti zao.

Mratibu wa Utafiti na Machapisho SUA Prof Japhet Kashaigili  akizungumza na watafiti (hawapo pichani)

Amesema wao kama waratibu wa mafunzo hayo wanakipongeza chuo kwa kuhakikisha kinatoa rasimali mbalimbali ili kuhakikisha kinakuwa na watafiti bora.

Akitoa salamu za shukrani kwa mgeni rasmi mmoja wa washirki wa mafunzo hayo Dkt. Halima Mangi amesema watahakikisha wanatumia mafunzo hayo kufanya tafiti bora na kusimamia miradi ya utafiti kikamilifu kwani wamepata elimu itakayowasaidia kufanya tafiti zenye tija.

 Dkt. Halima Mangi akitoa neno la shukrani

Mafunzo hayo yameshirikisha watafiti wachanga 27 ambapo wamejifunza namna bora ya kufanya utafiti, kuandika miradi ya kitafiti, kutafuta wafadhili wa miradi  na namna bora ya kusimamia miradi hiyo.

Picha chini na matukio mbalimbali na upokeaji wa vyeti.







Post a Comment

0 Comments