Na: Gerald Lwomile, Dodoma
Imeelezwa kuwa pamoja na kuwepo
kwa mashirikiano wakati wa kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo
(ASDP) awamu ya I na ya II, kumekuwa na changamoto kwa wadau wake ikiwa ni
pamoja na kutokuaminiana na baadhi ya wadau wa programu hiyo kutokuwa na uwezo
stahiki.
Mtafiti na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Emmanuel Malisa akiwasilisha matokeo ya utafiti |
Haya yamesemwa Aprili 13, 2023
Jijini Dodoma na Mtafiti na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) Dkt. Emmanuel Malisa wakati wa mawasilisho ya matokeo ya utafiti wa
Mashirikiano ya Wizara Mama za Sekta ya Kilimo katika Mapinduzi ya Kilimo
Tanzania.
Dkt.
Malisa amesema kuwa kwa ujumla mashirikiano yapo kati ya wadau wa ASDP.
Wanashirikiana kwa namna mbalimbali ikiwemo ubadilishanaji wa taarifa au
rasilimali mbalimbali zinazohusiana na kilimo, kama vile taarifa za kitaalamu
kuhusu umwagiliaji, uzalishaji wa mazao na mifugo, masoko na hata taarifa za
mlipuko wa magonjwa au wadudu waharibifu wa mazao au mifugo. Njia inayotumika
zaidi ni mikutano rasmi na ya mwisho ni barua pepe.
Wadau mbalimbali walioshiriki katika uwasilishaji wa matokeo ya utafiti |
Akizungumzia
ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa ASDP yakiwemo Mashirika yasiyo
ya Kiserikali yaani NGOs na makampuni yanayofanya kazi na wakulima, Dkt. Malisa
amesema wadau hao wamekuwa na mashirikiano duni baina yao na hiyo inasababishwa
na kutokuwepo na mpango bora wa uratibu na kuwa yangekuwa na nguvu zaidi endapo
yangekuwa katika utaratibu mzuri wa kubadilishana uzoefu na yangechangia vizuri
zaidi katika utekelezaji wa ASDP.
Aidha
Dkt. Malisa amesema katika utafiti wameona upungufu wa maafisa ugani ukilinganisha
na idadi kubwa ya wakulima na hivyo inakuwa ni vigumu kuwafikia wakulima wote.
Pia, maafisa ugani hao hawana mafunzo ya mara kwa mara ya kuongeza ujuzi.
Amesema
imeonekana kuwepo kwa malalamiko kwa baadhi ya watendaji katika sekta ya kilimo,
ambao wapo chini ya TAMISEMI wakidai kurejeshwa katika Wizara ya Kilimo.
Mtafiti huyo alisema kuna uwezekano mkubwa kwa watendaji wenye malalamiko kama
hawa kutoshishiriki kwa moyo wa dhati katika utekelezaji wa ASDP, ingawa
machoni wanaonekana wanashirikiana na wadau wengine.
Vikundi
vya wakulima, ambavyo ndio walengwa wa programu vimeonekana kutokuwa imara na
hivyo kuwepo changamoto katika upokeaji wa elimu na maelekezo mbalimbali na
utekelezaji wake. Dkt. Malisa ameongeza kuwa hata waratibu wa ASDP nao hawana
motisha stahiki wa kutekeleza majukumu yao ya uratibu kwani wanajiona kuwa
hawathaminiwi vya kutosha.
Dkt. Malisa amesema, kwa baadhi
ya wadau, msukumo wa mashirikiano yao unatokana na hofu ya kuchukuliwa hatua za
kisheria kama watumishi wa umma na si utashi wa kutoka ndani au nia ya kuleta
matokeo, jambo ambalo limepelekea kushindwa kuchangia kikamilifu katika
utekelezaji wa programu hiyo na hivyo kusababisha kutopatikana matokeo chanya
kwa kiwango kilichotarajiwa.
Amesema
mashirikiano ni ya lazima katika utekelezaji wa mipango inayohusisha watendaji /
wadau wengi na inayotarajiwa kuleta matokeo ya pamoja. Lakini si wakati wote
mashirikiano yanaleta matokeo chanya. Unawezakuta wadau wanashirikiana lakini
matokeo sio chanya. Mashirikiano yanawezakuwa yenye kuweka nguvu pamoja kwa nia
moja na hivyo kuleta matokeo chanya au yakawa yaliyogubikwa na misuguano na
kutoaminiana kati ya wadau na hivyo kutoleta matokeo ya pamoja tarajiwa.
Kutokana
na matokeo ya utafiti huo, Dkt. Malisa amesema kuwa wao kama watafiti wana
pendekezo la kisera lifuatalo: Ili mashirikiano ya wadau wa ASDP yaweze kuwa yenye
kuweka nguvu pamoja kwa nia moja na hivyo kuleta matokeo chanya, ni vema wizara
mama za sekta ya kilimo (agricultural sector lead ministries) na wadau wengine wa
ASDP wakawekeza kuhakikisha kuwa wadau hao wana uwezo wa kitaasisi, ki-fedha na
ki-utendaji; wana uelewa wa kanuni na taratibu za utekelezaji wa vipaumbele vya
ASDP; wana motisha (wanashirikishwa kikamilifu, wanaratibiwa sawasawa na
matarajio, kanuni zilizopo zinasimamiwa ipasavyo); na wanaamiana.
0 Comments