Na: Tatyana Celestine
Katika kuhakikisha tafiti za masuala ya misitu, kilimo na mifugo zinaendana na mabadiliko ya tabianchi Chuo cha Sokoine cha Kilimo kimezindua Mashine ya Kuchakata Mazao ya Misitu aina ya “Slidetec Sawmill 2020” yenye thamani ya takribani sh, milioni 200.
Mashine hiyo imezinduliwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji Mstaafu Joseph Warioba Jijini Arusha katika Msitu wa Mafunzo wa Olmotonyi na kuwataka wajumbe wa Baraza la Chuo wahakikishe tafiti za masuala ya misitu, kilimo na mifugo zinazofanywa chuoni hapo ziendane na mabadiliko ya tabia nchi na zitatue changamoto nchini.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA, Profesa Raphael Chibunda amesema kuwa uwepo wa mashine hiyo utasaidia uboreshaji wa mafunzo kwa vitendo kwa kiasi kikubwa kwani ina uwezo wa kuchakata mita za ujazo 10 hadi 15 kwa saa 8 tofauti na ilivyokuwa awali ambapo mashine ilikuwa inachakata mbao mita za ujazo 5 hadi 7 kwa saa 11.
Prof Chibunda amesema kupitia Msitu wa Mafunzo wa Olmotonyi umeweza kuwa chanzo cha utunzaji wa vyanzo vya maji vya Mlima Meru, kutoa ajira kwa vibarua zaidi ya 60 hivyo kupelekea mapato ya sh. milioni 700 hadi sh. bilioni moja kwa mwaka kama ambayo yametokana na mazao yatokanayo na msitu huo.
Akizungumzia faida ya kuwepo kwa mashine hiyo chuoni hapo Kaimu Rasi Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii, Dkt. Agnes Sirima amesema mashine hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji kwa Chuo pamoja na kufundisha wanafunzi wa Shahada ya Misitu, Teknolojia ya Misitu na Uongezaji wa Thamani kwani uwiano wake ni mkubwa wa kuzalisha mbao na kutumia treka kwa ajili ya kuchana mbao endapo umeme ukikatika.
Uzinduzi huo ulienda sambamba na kufungua Mafunzo ya Uongozi kwa siku mbili tarehe 28-29, March 2023 ambayo yametolewa na Taasisi ya Uongozi kwa lengo la kuongeza tija katika utendaji ambayo yalihusisha wajumbe wa Baraza la Chuo pamoja na Washiriki wa Menejiment ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.
0 Comments