Na: Amina Hezron,Morogoro.
Wadau wa zao la Soya, Kahawa, Miwa
na Nyama pori wametakiwa kushiriki kikamilifu kwenye kutoa mapendekezo na maoni yao kwenye Mradi wa Utafiti wa Biashara, Maendeleo na Mazingira (TRADE Hub) ili matokeo yatakayopatikana yaweze
kuinua tija uchumi nchini.
Hayo yameelezwa na Kaimu Rasi wa
Ndaki ya Uchumi na stadi za Biashara Dkt. Zena Mpenda aliyemuwakilisha
Rasi wa Ndaki hiyo Dkt. Damas Philip katika
warsha iliyoandaliwa na mradi huo ili kuwasilisha matokeo ya awali ya
utafiti wao kwa wadau ili kupata maoni yao
juu ya namna bora ya kufanya biashara ya haki na endelevu.
Amewataka wadau hao kuzingatia
kuwa tasnia hizo zinagusa kwa namna moja ama nyingine maisha na maendeleo ya
wadau mbalimbali pamoja na uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla hivyo watumie
fursa hiyo kwa makini kutoa maoni yao ya namna bora ya kuboresha biashara katika tasnia hizo zote za Nyama pori na Mazao
ya kilimo.
“Ni vizuri tunaposikiliza hizi
mada zinazotolewa tuangalie inaelezea kweli ile hali halisi kwenye maeneo yetu
ili tuweze kuboresha yale ambayo tumeyaona lakini pia tuweze sasa kuangalia
mapendekezo yanayotoka tuone hayo mapendekezo yatafanyika yanawezekana ili
tukitoka hapa tuwe na mapendekezo ambayo ni bora zaidi”, alisema Dkt. Zena.
Dkt. Zena ameeleza kuwa Serikali
imekuwa ikiboresha mara kwa mara Sheria, taratibu na Kanuni kuhakikisha kwamba
biashara hizo hazisababishi ongezeko la uharibifu wa mazingira na upotevu wa
baionuai hivyo ni muhimu kama wadau wa biashara kuhakikisha wanaingia kwenye
mikataba ya kijani kwenye biashaa zao ili kuwe na biashara endelevu kwaajili ya
watu na ulimwengu pia.
Akieleza malengo ya warsha hiyo
Mratibu wa Utafiti na Machapisho (SUA) Prof. Japhet Kashaigili amesema kuwa ni
kuwasilisha kwa wadau matokeo ya tafiti kadhaa ambazo mradi huo umeyapata ili
wapate nafasi ya kuyajua, kuyajadili na kutoa mapendekezo ili kuona ni namna
gani yanaweza kuchangia kwenye maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
“Lengo lingine la pili la warsha yetu hii na mradi ni kutengeneza mpango au njia itakayotupeleka nchi mahali fulani kuptia ufanyaji wa biashara yenye haki na endelevu nchini Tanzania lakini pia bidhaa zetu ziweze kuhimili ushindani kwenye masoko ya kimataifa na kukuza uchumi”, alifafanua Prof. Kashaigili.
Aidha amesema dhumuni kubwa
linalobeba mradi huo ni kuhakikisha biashara ya mazao na nyama pori inakuwa ni
injini ya ukuaji wa uchumi jumuishi,Kuondoa umasikini na kama mbinu ya
kutekeeleza maendeleo endelevu kama ilivyosisitizwa kwenye Mpango wa maendeleo
endelevu bila kuchangia uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa mradi huo
Prof. Reuben Kadigi amesema warsha hiyo ya wadau ni muhimu sana katika kupata
maoni na mapendekezo ambayo yatawasaidia watafiti kuweza kutengeneza andiko la
sera ambalo litawasilishwa Serikalini ili kusaidia kufikia malengo
yaliyokusudiwa.
“Kila mchango wa mdau
unaotolewa andika mahali kila ushairi andika ili mwisho wa siku tupate kitu
kizuri kifupi cha kuwasilisha serikalini baada ya kufanya uchambuzi wa kina
kulingana na matokeo tuliyoyapata maana mwisho wa siku hatuwezi kupeleka kwa
watunga sera kitu kinacholeweka nawaweze kukifanyia kazi kwa ustawi wa biashara
nchini”, alieleza Prof. Kadigi.
Kwa upande wake Dkt. Charles
Malaki aliyemuwakilisha Kaimu Rasi wa Ndaki hiyo amewashukuru wadau
waliojitokeza katika warsha hiyo na amewataka kutoa maoni na mapendekezo ya
kuboresha matokeo ya tafiti hizo ili kuisaidia Serikali baadae kupata sera bora
zitakazosaidia kuwa na uendelevu katika biashara ambayo inajali Mazingira,Nyama
pori pamoja na watu.
Mradi wa Utafiti wa Biashara,Maendelo
na Mazingira (TRADE Hub)ni mradi wa miaka mitano unaotekelezwa na Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na washirika wengine kutoka katika
nchi kumi na tano za Afrika, Asia, Uingereza
na Brazil kuanzia Februari 2019 hadi Machi 2024.
0 Comments