Na: Calvin Gwabara – Iringa.
Wafanya biashara hususani wauzaji
na wachoma Mahindi mabichi kwenye eneo maarufu la Mlima Kitonga Mkoani Iringa
wamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
kupitia Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Mkuu wa Mkoa
huo Mhe. Halima Dendego kuona uwezekano wa kuwajengea vibanda maalumu vya
kufanyia biashara katika eneo hilo ili kuweza kufanya biashara hiyo vizuri
katika msimu wa mvua na kiangazi na kujipatia kipato cha kuendesha familia zao.
Abiria wanaosimama na kujipatia mahindi mabichi ya kuchoma katika eneo hilo Maarufu la Mlima Kitonga. |
Wakiongea na SUAMEDIA katika eneo hilo Mmoja wa
wafanyabaishara hao bwana Yackonia Monyi wamesema eneo hilo ni moja kati ya
maeneo maarufu sana kwa wasafiri wanapitia njia hiyo kwenda mikoa yote ya
nyanda za juu kusini kusimama na kuburudika kwa kununua mahindi fresh kutoka
shambani tofauti na maeneo mengine ambayo wanauza mahindi yaliyokaa hata wiki
na kupoteza ladha.
“Ndugu Waandishi hapa ni sehemu
ya mapunziko kwa wanaumaliza kupanda mlima huu mkali na maandalizi ya moyo ya
wanaoshusha mlima huu mkali,kwahiyo wanakula mahindi choma fresh kabisa na
kununua na bidhaa kama zawadi za kupeleka wanapokwenda na nikuhakikishie hapa
wanasimama Mwaziri,Wabunge, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Mabalozi na viongozi
wengne wakubwa Serikalini lakini mazingira ya hapa ni mabaya sana nyakati za
mvua watu wanashindwa kusimama na sisi biashara inakuwa ngumu sana na wateja
wanakosa kula mahindi na vitu vingine, tuombe Rais wetu mama yetu Mhe. Dkt.
Samia atusaidie na sisi maana Mzee wetu Magufuli aliwajengea wale wa Dakawa
kule Morogoro” alisema bwana Monyi.
Nae kwa upande wake bwana Meddy
Magubika Amesema hilo limekuwa eneo maarufu zaidi kwa uchomaji wa mahindi
yasiyo lala na matamu ndio maana yanasimama magari makubwa na madogo na hata
mabasi ili kuwapa nafasi wasafiri wao kula mahindi mazuri na kuendelea na
safari.
“Hapa kwetu tunaamka usiku sana
kuingia shambani kuvuna mahindi haya mabichi na ikifika saa moja asubuhi
unakuta tayari tushafika na watu wanakula mahindi ya kuchoma na wengune
wanabeba kwaajili ya kupeleka zawadi majumbani kwao, hapa mahindi yasiyoalala
hatuuzi kwakuwa tunalinda soko letu lisiharibike ili tunaedelee kupata soko na
kubaki na umaarufu wetu” alieleza bwana Magubika.
Aliongeza “Kila mtu anayeanza
safari kupita njia hii kwenda Njombe, Songea, Mbeya, Tunduma, Katavi, Rukwa awe
dereva wa magari makubwa, mabasi, magari madogo na wanautumia usafiri binafasi
anayejua eneo hili lazima awaze kula mahindi ya kuchoma katika eneo hili sasa
akipita wakati mvua inanyesha kubwa hawezi kufungua dirisha kuchukua mahindi
wala kushuka na kwa maana hiyo sisi tunapoteza hela mahindi yanabaki tunatupa
na kupata hasara”.
Nae Mfanyabishara mwingine bwana
Kasian Yuda amesema biashara ya mahindi wanayoifanya inawasaidia katika kumudu
mahitaji mbalimbali ya familia zao kama vile kusomesha watoto, kujenga nyumba
na mahitaji mengine ya binadamu hivyo biashara hiyo wao wanaiona kuwa ni kazi
rasmi katika maisha yao kwakuwa wengine wameianza miaka mingi na maisha
yanakwenda.
“Unavyotuona hapa sisi wengine
tumeridhi kazi hii hapahapa kwa wazazi wetu, tunachoma mahindi na kuuza maana
sio kila mtu lazima awe mkulima wengine hatulimi lakini tunasaidia wakulima
kupata soko la mazao yao kwahiyo tunategemeana wao wanapata hela na sisi
tunapata kwa kuuza mazao yao na kuendeleza maisha yetu kwahiyo serikali
ituangalie sisi kama vijana tulioamua kujiajiri katika kilimo kwa njia hii”
alisema bwana Yuda.
Aidha wameomba eneo hilo
kuboreshwa kwa maana ya kuongezewa pia nafasi au kuhamishiwa sehemu nzuri
kuwezesha magari mengi zaidi kusimama na kupata huduma kwakuwa eneo hilo ni
dogo na hufika wakati magari mengine hushindwa kusimama kwakuwa panakuwa
pamejaa na hawawezi kusimama katikati ya barabara kutokana na eneo hilo kuwa
hatari kwa magari yanayopita kushuka au kumaliza kupanda mlima huo mkali.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akihimiza vijana wengi kujiajiri
katika kilimo kwa kuingia katika mnyororo wa thamani kama ambavyo vijana hao
wamefanya hivyo kilio chao kikisikiwa na kutatuliwa kitasaidia kupunguza tatizo
la ajira kwa vijana kwenye eneo hilo la kitonga maarufu kwa uchomaji wa mahindi
mabichi nchini na kuongea usalama kwa abiria na abiria wanaosimama eneo hilo
kula mahindi mabichi kutoka shambani.
PICHA ZA ENEO LA UCHOMAJI WA MAHINDI MLIMA KITONGA IRINGA.
0 Comments