Na Gladness
Mphuru
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amewaasa watanzania wote hususani vijana kuchangamkia fursa za kilimo ili kujiajiri na kuwa na usalama na uhakika wa chakula nchini.
Ametoa kauli hiyo akiwa Mubashara katika kipindi cha Mizani cha TBC katika ukumbi wa Baraza la Chuo Kampasi Kuu ya Edward Moringe mkoani Morogoro, kikiwa na mada isemayo Vijana na Fursa za Kilimo, ambacho kimehusisha Wanataaluma, Vijana Wahitimu na wanaoendelea na masomo SUA.
Prof. Chibunda ameishukuru Wizara ya Kilimo kupitia Waziri mwenye dhamana Mhe. Hussein Bashe kwa kuanzisha mpango mkakati wa 'Building a Better Tomorrow' (BBT) kwani wahitimu na wanaoendelea na masomo chuoni hapo wamechangamkia fursa hiyo yenye lengo la kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana nchini.
" Lakini kwenye huu mpango wa BBT vijana wetu ambao ni wahitimu wa Chuo hiki hata wale ambao bado hawajahitimu kwa sehemu kubwa sana wameupokea na kutuma maombi ili waweze kushiriki kwani kwa awamu ya kwanza Wizara ilitoa nafasi elfu moja lakini maombi yamepindukia elfu ishirini”.
Aidha Prof. Chibunda ameiomba Serikali iondoe kodi katika Sekta ya Kilimo ili vijana watimize ndoto zao na kusema kuwa vijana watakaopata fursa za kilimo wasimuangushe Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zaidi wakawe waaminifu na kufanya kazi kwa bidii ili kunufaika.
Kwa upande wake Dkt. Fulgence Mishili Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na Mtaalamu wa Kilimo Biashara amesema, mkakati huo ni bora kwa Serikali na vijana kwa sababu utatengeneza fursa za kilimo kupitia mnyororo wa thamani wa kilimo cha kuanzia shambani hadi sokoni hivyo itatoa ajira nyingi kwa vijana ili kusaidia kuongeza pato la Taifa.
Naye Mwita Mroni ambaye ni Mhitimu wa SUA amesema kuwa Serikali kupitia mpango huo ni maono ambayo kama yakitekelezeka vyema utawasaidia vijana pamoja na Taifa kuwa na kilimo endelevu ambacho kitachangia kukuza Pato la Taifa.
Mwita Mromi ambaye ni Mhitimu (SUA) akishiriki kipindi cha Mizani cha TBC. |
Dkt. Fulgence Mishiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Mtaalam wa Kilimo Biashara akishiriki kipindi cha Mizani cha TBC. |
0 Comments