Na. Vedasto George.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Chama cha Wafanyakazi SUA Main Administrative Staff Community (SUMASCO) wamefanya ziara ya siku mbili ya kutembelea vivutio vya utalii katika Hifadhi za Udzungwa na Mikumi kwa kujifunza na kujionea vivutio vilivypo nchini ikiwemo kuongeza pato la Taifa.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi SUMASCO Bi Josephine Lwiza amesema kuwa Watanzania wametakiwa kujiwekea mazoea ya kufanya Utalii wa ndani mara kwa mara katika kuhakikisha vivutio vya utalii vilivypo hapa nchini vinatangazika na kuwa mabalozi wazuri wa kutangaza maeneo ya utalii yaliyopo katika hifadhi zilizopo nchini.
“ kuna mambo mengi ya kujifunza sisi SUMASCO leo tumetembelea Udzungwa na Mikumi lakini pia siku nyingine tutaenda katika hifadhi nyingine na yote haya tunayafanya ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutangaza vivutio vya utalii.”Amesema Josephine Lwiza.
Aidha ameishukuru Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuendelea kutoa fursa kwa watumishi wake kwenda kufanya utalii wa ndani na kuwa jambo ilo litasaidia kuongeza utendaji kazi katika Taasisi hiyo kwa kuzingatia moja ya shughuli zinazofanya na Chuo ni pamoja na masuala ya utalii.
Kwaupande wao Bw. Anderson Charles na Bw. Omar Tunga kutoka SUA wamesema kwa muda mrefu SUMASCO kama Chama kimekuwa kikifanya shuguli za utalii katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa dhumuni moja la kuiunga mkono Serikali katika kutangaza utalii uliopo nchini.
“Tumefanya hivi kutembelea maeneo ya utalii wakati tunajiandaa na kikao chetu cha mwaka na tunatarajia kwenye kikao hicho kubadili katiba yetu ili iweze kuwa rafiki na madhumuni ya umoja wetu ni kusaidiana pale mtumishi mwenzetu atakapo pata shida”. Amesema Bw. Tunga
Naye Charles Kisangilo ambaye ni muongoza watalii Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa amebainisha maeneo yaliyotembelewa kuwa ni Maporomoko ya maji Sanje na maeneo ya kihistoria pamoja na Msitu wa Udzungwa.
Aidha Bw. Karoli Shirima ambaye pia ni muongoza watalii katika hifadhi ya Taifa Mikumi alipokuwa akitoa historia ya jinsi ya kuanzishwa hifadhi hiyo amesema kuwa Hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka 1964 ikiwa na Kilometa za Mraba zipatazo 1070 lakini ilipofika mwaka 1970 hifadhi hiyo iliongezwa ukubwa na kuifanya hifadhi hiyo kuwa na ukubwa wa kilimeta 2330.
Ameongeza kuwa Hifadhi ya Taifa Mikumi kwasasa ni hifadhi ya tisa kwa ukubwa baada ya kuongezwa vijiji vilivyokuwa Jirani na hifadhi hiyo pia ameongeza katika hifadhi hiyo kuna jamii mbalimbali za Wanyama ikiwemo Simba, Tembo,Twiga na Swala.
0 Comments