SUAMEDIA

Miradi ya kimkakati ina mchango mkubwa kwa Maendeleo ya Taifa- Naibu Waziri Mathew


Na: Farida Mkongwe

Maafisa Mawasiliano wamekumbushwa kutimiza wajibu wao wa kutoa Elimu kwa Umma kuhusu umuhimu wa Miradi ya Kimkakati ambayo inatakiwa itazamwe kwa jicho la kidigitali ili kuendana na mabadailiko ya kidunia.


Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akifungua Mkutano wa 107 wa Washitiri wa Vipindi vya Elimu kwa Umma unaofanyika mjini Morogoro.

Kauli hiyo imetolewa Februari 21, 2023 na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew wakati akifungua Mkutano wa 107 wa Washitiri wa Vipindi vya Elimu kwa Umma unaofanyika mjini Morogoro.

Mhandisi Mathew amesema Maafisa Mawasiliano ndio daraja kubwa kati ya Serikali na wananchi na kwamba wana wajibu mkubwa wa kuandaa Vipindi vya Elimu kwa Umma kuhusiana na Miradi ya Kimkakati ambayo inachangia maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kiasi kikubwa.

Aidha Naibu Waziri huyo amewakumbusha Washiriti wa Vipindi vya Elimu kwa Umma kuendelea kuielimisha jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanatishia ustawi wa dunia.

“Dunia inakumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, ninyi kama Wataalamu wa Mawasiliano mna jukumu la kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa Mazingira, andaeni vipindi vya Elimu kwa Umma ili watu waepukane na vitendo hatarishi vya uharibifu wa misitu na vyanzo vya maji”, amesema Mhandisi Mathew.

Kwa upande wao baadhi ya Washitiri akiwemo Hadija Maulid ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko Chuo Kikuu Ardhi na Geophrey Mlewa ambaye ni Mwakilishi wa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao wamesema mafunzo wanayoendelea kuyapata ni muhimu kwao kwa kuwa yanawaongezea maarifa ya namna bora ya kuwasiliana na jamii. 



Post a Comment

0 Comments