SUAMEDIA

Baraza la Madiwani simamieni Mapato na Miradi ya Maendeleo - Rebecca Nsemwa

 Na: Winfrida Nicolaus

Baraza la Madiwani Manispaa ya Morogoro wametakiwa kuhakikisha wanaboresha na kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa Mapato ndani ya Manispaa pamoja na kukamilisha Miradi yote ya Maendeleo ndani kwa wakati na thamani ya pesa kuonekana.


Mkuu wa Wilaya Bi. Rebecca Nsemwa akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Morogoro (Picha zote na Winfrida Nicolaus)

Hayo yamebainishwa Februari 8, 2023 mkoani Morogoro na Mkuu wa Wilaya Bi. Rebeca Nsemwa wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Baraza la Madiwani Manispaa ya Morogoro uliofanyika katika Ukumbi wa Manispaa Mkoani Morogoro.

Amesema katika mpango walionao wa kuhakikisha Manispaa ya Morogoro inakuwa Jiji ni swala la mchakato ambao unahitaji ushirikiano madhubuti baina ya Madiwani, Watendaji pamoja na Wataalam na ushirikiano huo unaanzia katika Nyanja ya ukusanyaji wa mapato kikamilifu.

Amesema Manispaa kuwa Jiji lazima vigezo vizingatiwe ikiwemo ukamilishaji wa Miradi kwa asilimia miamoja kama vile Vituo Bora vya Afya, Hospitali, Zanati zilizokidhi vigezo, Shule kwa maana ya Msingi na Sekondari hata Miundo mbinu mizuri na vyote hivyo ili kukamilika inahitaji jitihada za kutosha pamoja na ushirikiano thabiti baina ya watendaji ndani ya manispaa.

“Ni lazima tuhakikishe tunasimamia Mapato yetu vizuri na ni lazima tukusanye Mapato ya kutosha na Mungu akijalia nitaweka oparesheni maalum ya kupita katika vyanzo vyote vya mapato kwa kushirikiana na wataalam wetu ili kupata picha kamili ikiwezekana kurekebisha palipo kosewa na cha muhimu zaidi baada ya ukusanyaji wa mapato hayo kinachofuata ni kusimamia matumizi bora ya mapato ili kufikia lengo”, amesema Mhe. Rebeca Nsemwa

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Bw. Ally Malechela amesema kwa mwaka huu wa fedha Manispaa imeibua vitega uchumi vingine vipya ili kuongeza mapato ikiwemo Mashine Mpya za kisasa kwa ajili ya ukusanyaji wa Mapato hayo vilevile kujenga ukumbi mkubwa ambao una uwezo wa kuweka watu 1500 hadi 2000.


Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Bw. Ally Malechela akizngumza na Madiwani katika Baraza la Madiwani Manispaa ya Morogoro

Ameongeza kuwa katika upande wa Miradi Baraza limedhamiria kwenda kukamilisha Miradi hiyo kwa wakati ambapo kwa mwaka wa fedha wa sasa na ujao watahakikisha hakutakuwa na mwanafunzi yeyote  atakaye kaa chini wakati wa masomo ndani ya Manispaa ya Morogoro,  vilevile kukamilisha Miundo mbinu kwa maana ya kuhakikisha wanafungua Barabara zote ambazo hazijafunguliwa na kutengeneza Mifereji mikubwa ili kuzuia Mafuriko.


Baadhi ya Madiwani wakisikiliza hotuba ya Mkuu wa Wilaya (hayupo pichani) kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Morogoro

Post a Comment

0 Comments