Adam Maruma - Dodoma
Maafisa mifugo nchini wametakiwa kuwahamasisha
wafugaji, kuchanja mifugo ili kuilinda dhidi
ya magonjwa mbalimbali ambayo yanatajwa kuwa ni moja ya kikwazo kikubwa kinachorudisha
nyuma maendeleo ya mifugo nchini.
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari ya Mifugo nchini Prof. Esron Karimuribo (kushoto) akipokea chanjo kutokwa kwa Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania Prof. Hezron Nonga
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania
chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga wakati akimwakilisha
Katibu Mkuu wa Wizara Hiyo, wakati akipokea chanjo za kuzuia magonjwa
mbalimbali ya Mifugo nchini ili kuunga
mkono jitihada za Chama cha Madaktari wa Mifugo nchini, watakaotoa huduma za elimu,
chanjo na upasuaji wa mifugo kwenye Kata za Nala na Mbalawala zizizo nje kidogo ya
Jiji la Dodoma .
Prof. Nonga amesema idadi ya mifugo nchini iliyochanjwa bado ni ndogo kwani katika Halmashauri 184 nchini ,kuna baadhi ya Halmashauri hazichanji
kabisa mifugo yao, lakini Madaktari wa mifugo wapo katika kata hizo, chanjo
zipo na wafugaji wapo tayari kuzilipia huku akitaja sababu kuwa ni kutowajibika
ipasavyo kwa baadhi wa Madaktari ya mifugo na maafisa ugani mifugo katika Halmashauri
hizo.
Mkurugenzi huyo wa Huduma za Mifugo nchini, ameongeza
kuwa ni muda wa Madaktari wa Mifugo nchini kufanya kazi kwa kujituma, kwani
katika kata 3,956 nchini na vijiji zaidi 12,193 nchi nzima, nusu ya kata hizo
zina maafisa mifugo ambao kwa wastani afisa mmoja anaweza kuhudumia vijiji
angalau 2 hadi 3 katika kata moja, na kuweza kutoa elimu ya namna ya kudhibiti
magonjwa ya Mifugo bila tatizo kwa kuwa wizara imewapatia pikipiki zaidi ya 300, huku pikipiki 1,200
zikitarajiwa kutolewa mwaka huu kwa
maafisa ugani wa mifugo, na madaktari hao ili waweze kufanya kazi yao kwa
urahisi.
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga akizungumza na wadau mbalimbali wa mifugo wakati akipokea chanjo hizo
‘’Wizara imeanzisha utaratibu wa kupima ufanyaji kazi
wa maafisa ugani mifugo na madaktari wa mifugo, kuona kama uwepo wao kazini una
tija kwa Serikali au wapo pale kwa ajili ya kupumzika huku Serikali ikendelea
kulipa mshahara kwani Serikali haipo tayari kuendelea kulipa Misahara kwa
wafanyakazi waliokuja kupumzika makazini
’’, Amesema Prof, Nonga.
‘’Nishukuru kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi
chache zinazozalisha chanjo yake yenyewe, sasa hivi kuna viwanda vitatu vya
kuzalisha chanjo ya mifugo, kuna kiwanda cha Serikali kinaitwa Tanzania Vaccine
Insitute, chini ya Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania, na kinazalisha Zaidi ya chanjo saba dhidi ya
magonjwa kipaumbele”
Amezitaja chanjo hizo kuwa ni zaidi ya dozi milioni 65
kwa mwaka na hizi zinatumika mara moja na kuisha , Kiwanda binafsi cha NOVABI kinazalisha
chanjo inaitwa Tatu Moja ambayo ni chanjo kuku na imeunganisha magonjwa matatu ya kuku ndani
yake ambayo ni Kideri, Ndui ya Kuku, pamoja na Mafua ya Kuku.
Chanjo nyingine zinazozalishwa ni dozi milioni 50 kwa
mwaka na kiwanda cha Wazalendo, lakini zaidi
ya yote kuna kiwanda kikubwa Kusini mwa Jangwa la Sahara ambacho kinaitwa Hester Biosciences Africa
Limited kiko Tanzania na kinatambuliwa na Dunia nzima na kinazalisha chanjo
aina 37 dhidi ya magonjwa mbali mbali ya mifugo.
Kwa upande Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari ya Mifugo
nchini Prof. Esron Karimuribo amewashukuru wawakilisha wa kampuni zilitoa
chanjo mbali mbali za mifugo na namna itakavyotumika katika kuhudumia wafugaji wa
kata za Nala na Mbawala zilizo nje
kidogo ya jiji la Dodoma na kusema zaidi ya dozi 4,000 zitatumika kuchanja mifugo katika kata hizo.
0 Comments