SUAMEDIA

Wilaya ya Mbarali yaishukuru SUA kwa kuichagua kuwa sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira

 Na Amina Hezron, Mbeya

Katibu Tawala wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Michael Semindu amekishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuichagua wilaya ya Mbarali kuwa sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira (EFLOWS) na kuwa sehemu ya mafunzo kwa wadau wengine.

Katibu Tawala Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Michael Semindu akizungumza na washiriki wa mafunzo wakati akihitimisha mafunzo hayo,Kulia ni Mkuu wa Mradi wa EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili.

Shukrani hizo amezitoa mara baada ya kufunga mafunzo ya Kimataifa ya siku tano ya kuwajengea uwezo Wanasayansi, Mameneja na wadau wengine namna ya kuendesha na kufanya tathimini ya Maji kwa Mazingira katika ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi yaliyofanyika wilayani humo.

Katibu Tawala huyo wa wilaya amesema kuwa uwepo wa maji yanayotiririka katika mito unasaidia kwa kiasi kikubwa katika kilimo huku maji yanayokusanywa kupitia bonde la Mto Rufiji yanaelekea kwenye bwawa la Mwalimu Nyerere Kidatu na maeneo mengine yanayofanya uzalishaji wa umeme. 

“Hivyo mafunzo haya yanapokuja kwetu ni swala zuri sana yanatujengea uwezo yanatukumbusha wajibu wetu wa msingi na tayari tumeshaanza kufanya matengenezo ya bikoni ambazo zitakwenda kuwekwa wakati wowote ili kuweka mipaka ya kingo katika mito yote itakayowasaidia wananchi kufahamu mipaka yao na wapi pakufanyia shughuli zao ili waweze kuilinda mito yetu”, alisema Semindu.

Amesema utunzaji wa mazingira ya mito na bonde ni swala la kimkakati wilayani hapo kutokana na shughuli za uzalishaji zinazofanyika na hivyo  amewataka wadau waliopata mafunzo kuyachukulia mafunzo hayo kwa umakini mkubwa na kuyaweka kwa vitendo ili yakaweze kuzaa matunda katika jamii.

“Tumekuwa na mafunzo mengi ambayo baadhi yao wamekuwa wakiyaweka kuwa yakwao wenyewe sasa kama mafunzo haya yatakwenda kufanya kazi katika sehemu husika yatatusaidia sana, mazingira ni janga kubwa sana duniani lakini bado watu wetu wanaelimu chache tunahitaji kutoa elimu pana kwao lakini elimu tu isitoshe yale wanaojifunza yakafanyike kwa vitendo”, alisema Semindu .

Akizungumzia mafunzo yaliyotolewa na Mhadhiri Mwandamizi kutoka Idara ya Uhandisi Ujenzi na Rasilimali Maji kutoka katika Shule Kuu ya Uhandisi na Teknolojisa SUA Dkt. Winfred Mbungu amesema kuwa mafunzo hayo kama wadau watayazingatia na kwamba yatakwenda kuongeza ujuzi kwao na kuwaelimisha wengine.

“Licha ya wengine kuwa ni watafiti wengine ni watendaji kutoka kwenye mabonde ambapo kila siku shughuli zao za kawaida ni kutunza vyanzo vya maji na rasilimali maji lakini pia wanahusika katika kusimamia sheria na kuelimisha wananchi hivyo tumejaribu kuwaelimisha waweze kujitambua waone namna gani wanaweza wakatathimini na wanaweza wakashirikiana na wananchi kuweza kuboresha”, alisema Dkt. Mbungu.

Baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo washiriki wote walipewa vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo yaliyojumuisha washiriki wote waliohudhuria mafunzo hayo kwa njia ya mtandao kutoka mataifa mbalimbali na wale walioshiriki moja kwa moja kutoka Tanzania.

Mratibu wa Mradi wa EFLOWS Dkt. Winfred Mbungu akieleza malengo ya mafunzo hayo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kutoa vyeti na kuyahitimisha.



Katibu Tawala Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Michael Semindu,(katikati waliokaa),Mratibu wa Mradi wa EFLOWS Dkt. Winfred Mbungu,(kushoto waliokaa) ,Mkuu wa Mradi wa EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili (wa kwanza kulia waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo.







Post a Comment

0 Comments