Na Faraja Masinde, Mtanzania Digial
Watanzania wamehimizwa kuchangamkia fursa mbalimbali za
kiuchumi zikiwamo za kilimo ambazo zinapatikana nchini Brazili.
Wito huo umebainishwa leo Agosti 31, 2022 na Balozi wa
Tanzania nchini Brazili, Profesa Aderadius Kilangi kupitia mkutano ulioandaliwa
na Watch Tanzania kwa njia ya Zoom.
Balozi Kilangi ambaye alizungumza moja kw amoja kutoka
Brazili, amebainisha matunda ambayo Tanzania inaweza kuyapata kupitia
ushirikiano wake na nchi hiyo hususan katika sekta za kilimo, biashara,
uwekezaji na mifugo.
Balozi Kilangi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Vyombo
vya habari kwa njia ya Mtandao wa Zoom, kutokea nchini Brazili ambapo alitumia
fursa hiyo kueleza matunda ambayo Tanzania inaweza kuyapata kupitia ushirikiano
wake na Brazili.
“Miongoni mwa fursa ziliopo Brazili ni kwenye Sekta ya Kilimo
hasa cha Maharage ya Soya, Mtama na Mahindi ya Njano, kuna kampuni
tumewasiliana nayo kutoka China imekuja Tanzania, imeanza kulima Soya na
tunatarajia itaanza kulima Maharage ya Njano na Mtama, kwa hiyo Wakulima wetu
Tanzania wanaweza kuanza kulima mazao haya.
“Kwani kampuni hiyo imeishakuja nchini Tanzania na kwa
usimamizi wa Wizara ya Kilimo inaendelea na maandalizi ya kulima zao la soya
kwa kiwango kikubwa, ikitarajia kulima ekari 100,000.
“Lakini pia wakulima wetu wa Tanzania wanayofuirsa ya kuweza
kulima kwa wingi zao la soya na baadaye mtama na mahindi ya njano,” amesema
Balozi Kilangi.
Aidha, amebainisha eneo jingine kuwa ni la zana za kilimo
ambapo ubalozi ulitembelea kampuni kadhaa za kutengeneza zana za kilimo kwa
hatua zote, yaani zana za: kusafisha mashamba; kung´oa visiki; kulima; kupanda;
kupalilia; kumwagilia; kuvuna; kupaki.
“Zana za kilimo zinazotengenezwa Brazil kwa ujumla zinasifika
kuwa na ubora mkubwa, ubalozi unashauri kufanya ushirikiano wa karibu na
kampuni hizo ili ziweze kufika Tanzania na kusaidia kuboresha kilimo.
“Pia, Ubalozi unatoa wito kwa wadau mbalimbali wa kilimo
nchini Tanzania kuanzisha ushirikiano na makampuni ya Brazili ili kupata zana
bora na Madhubuti,” amesema Balozi Kilangi.
Pia Balozi Kilangi amegusia kilimo cha miwa na uzalishaji wa
sukari ambapo amesema kuwa nchi hiyo inafanya vizuri kwa kuwa kinara kwenye
uzalishaji wa sukari duniani.
“Ubalozi umefaulu kufanya ziara kwenye mojawapo ya viwanda vikubwa
vya kuzalisha sukari cha Uzina Coruripe mnamo Mei 2022, ambacho pia kinamiliki
mashamba makubwa sana ya miwa.
“Ulifanikiwa kuwashawishi kuangalia uwezekano wa kuwekeza
Tanzania kwa ubia au kwa njia nyingine yeyote, katika kilimo cha miwa na
uzalishaji wa sukari, na wahusika walionesha nia na utayari wa kufanya hivyo.
“Hivyo tunatoa wito kwa wadau wa kilimo cha miwa na
utengenezaji wa sukari nchini Tanzania kuangalia uwezekano wa kuitumia fursa
hii kwa kuanzisha ushirikiano na Brazili katika kukuza kilimo cha miwa na
uzalishaji wa sukari kwa kutumia teknolojia ya kisasa,” amesema Balozi Kilangi.
0 Comments