SUAMEDIA

Hospitali ya Rufaa ya Wanyama SUA kushirikiana na Manispaa ya Morogoro kutoa Elimu, Ushauri na Chanjo kuhusiana na Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa

 

Na: Gojo Mohamed

Katika kuhakikisha ugonjwa wa kichaa cha mbwa unadhibitiwa nchini Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Hospitali yake ya Rufaa ya Wanyama kwa kushirikiana na Manispaa ya Morogoro kimeweza kutoa elimu, ushauri pamoja na chanjo kuhusiana na ugonjwa huo katika Kata ya Bigwa na Mindu zilizopo Manispaa ya Morogoro.

Dkt. Isack Kashoma akitoa Chanjo ya Kichaa cha Mbwa kwa mnyama Mbwa Kata ya Mindu Manispaaa ya Morogoro katika zoezi la utoaji wa chanjo ya kichaa cha mbwa ikiwa ni Kampeni ya kitaifa kusisitiza umuhimu wa chanjo hiyo . (Picha na Gojo Mohamed).

Akizungumza katika zoezi hilo Septemba 28 mwaka huu, Daktari Mkuu wa Hospitali hiyo Isack Kashoma amesema ugonjwa wa kichaa cha mbwa unasababishwa na kimelea cha Kirusi na ni ugonjwa ambao unawapata Wanyama wafugwao kama vile mbwa, paka  ng’ombe, mbuzi na hata Wanyama pori kama vile fisi waking’atwa na mbwa mwenye ugonjwa huo.

Na sisi kama Hospitali ya Rufaa ya Wanyama tulipewa Kata mbili ambazo ni Mindu na Bigwa, katika kata ya Mindu tulikuwa na vituo vinne ambavyo ni Lugala,  Kasanga, Mindu sekondari pamoja na Madaganya na katika Kata ya Bigwa tulikuwa na vituo vinne ambavyo viliweza kutoa huduma hiyo na mwitikio ulikuwa ni nzuri”, amesema Dkt. Kashoma.

“Na katika Kata ya Mindu tumeweza kuchanja Wanyama si chini ya 140 huku Kata ya Bigwa wakichanja zaidi ya mbwa 200 na hili zoezi litaendelea hadi tarehe 2 mwezi wa 10 mwaka huu hadi pale kampeni ya kitaifa itakapo malizika”,  amesema Dkt.huyo.

Ameongeza kuwa anawakaribisha wafugaji ili waweze kupeleka mbwa wao katika Hospitali ya Rufaa ya Wanyama iliyopo SUA ili kuweza kupatiwa chajo ambayo inatolewa bure katika kipindi chote cha kampeni hii ya kitaifa na kusisitiza kuwa chanjo hii muhimu kwa sababu mbwa akishapata ugonjwa huu hawezi kupona.

Amesema binadamu anaweza kupata ugonjwa huu kupitia kung’atwa na mbwa mwenye kichaa au kugusa majimaji hasa mate ya mbwa mwenye ugonjwa huo.

Kwa upande wa Bi. Resti Longo na Bw. Kedimundi Ngewe  ambao ni wakazi wa Lugala wamekishukuru Chuo cha SUA kwa kutoa chanjo hiyo na kuwahamasisha wafugaji kujitokeza ili mbwa wao waweze kuchanjwa.

Zoezi hilo la utoaji wa chanjo ya kichaa cha mbwa limejumuisha baadhi ya Wanafunzi wanaosoma Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Tiba ya Wanyama na Mifugo kutoka SUA kwa lengo la kuwajengea uwezo na uzoefu katika masomo.

Mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Tiba ya Wanyama na Mifugo akishiriki kutoa Chanjo ya Kichaa cha Mbwa ili kuweza kuongeza ujuzi katika ikiwa ni Kampeni ya kitaifa.(Picha na Gojo Mohamed)




Mfugaji wa Mbwa akiwa anasubiria Mbwa wake waweze  kupatiwa  Chanjo ya Kuthibiti Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa katika Mtaa wa Lugala Kata ya Mindu Manispaa ya Morogoro. (Picha na Gojo Mohamed)




Paka aliyeletwa na kupatiwa Chanjo ya kuzuia Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa katika Mtaa wa Madaganya  Manispaa Ya Morogoro. (Picha na Gojo Mohamed) 


 

Dkt. Isack Kashoma akiwa na Bi. Resti Longo ambaye alimpeleka Mbwa wake kupatiae Chanjo ya Kichaa cha Mbwa katika Mtaa wa Lugala  Manispaaa ya Morogoro. (Picha na Gojo Mohamed)

Dkt. Isack Kashoma (aliyevaa Kofia)  katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Udaktari wa Wanyama na Mifugo baada ya zoezi la kutoa chanjo ya Kichaa cha Mbwa Manispaa ya Morogoro. (Picha na Gojo Mohamed)

 


 

 

Post a Comment

0 Comments