SUAMEDIA

SUA yazindua Kigoda cha Kitafiti cha Oliver Tambo cha Afrika

NA:Winfrida Nicolaus

Moja kati ya Vigoda 10 vya Kitafiti vya Oliver Tambo cha Afrika kinachohusu Magonjwa ya Kuambukiza yatokanayo na Virusi kwa Binadamu pamoja na Wanyama kimezinduliwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo SUA mkoani Morogoro kwa lengo la kuboresha Afya ya Binadamu pamoja na Mifugo.

Uzinduzi huo umefanyika Agost 15, 2022 mjini Morogoro  katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine iliyopo SUA.



Akifungua uzinduzi huo Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Juma Kipanga ambaye alikuwa Mgeni Rasmi akimwakilisha Mhe. Adolf Mkenda Waziri wa Elimu Sayansi, na Teknolojia amesema katika Kigoda hicho Cha Oliver Tambo kilichozinduliwa SUA kimewezesha upatikanaji wa fedha kwa njia ya ufadhili wa zaidi ya sh. Bilioni 2 ambazo zitaenda kusaidia katika kufanya tafiti mbalimbali hasa zile zinazojikita katika Magonjwa ya Kuambukiza yatokanayo na virusi kwa Binadamu na Wanyama 


Amesema  Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imeweza kuongeza fedha za Tafiti kutoka bilioni 3 mpaka bilioni 9 ili kuhakikisha kuwa Taasisi zote za Kielimu zinashirikiana na Tume ya Sayansi na Teknlojia COSTECH katika kuondoa tafiti zote zilizofanyika na zinazofanyika toka kwenye makablasha au maandishi na kuzipeleka kwenye matumizi Kwa lengo la kuisaidia Jamii.

"Kwa hiyo hapa SUA tutakuwa na Kigoda hiki ambacho kitashughulikia Tafiti kwenye maeneo haya ya Binadamu pamoja na Mifugo lakini ikumbukwe mwaka 2020 tulizindua Kigoda chetu cha kwanza ambacho kilizinduliwa katika Chuo Cha Nelson Mandela Jijini Arusha ambacho chenyewe kilijikita zaidi kwenye Binadamu pamoja na Mimea hivyo tunaamini kabisa kupitia Tafiti tunaenda kutatua changamoto ambazo Jamii yetu inakabiliana nazo", amesema Mhe. Omary Kipanga

Naye Mwenyekiti wa Kigoda Cha Utafiti Cha Oliver Tambo Prof. Gerald Misinzo kutoka Wakfu wa Utafiti na Udhibiti wa Magonjwa Ambukizi ya Afya moja  SACIDS, SUA amesema kuwa Kigoda hicho kina mkakati unaolenga kuikwamua nchi kutokana na magonjwa yanayoathiri ufugaji au mifugo pamoja na afya ya binadamu ili kuharakisha utekelezaji wa maono ya Tanzania ya Kimaendeleo na Bara la Afrika kufikia 2060 na utekelezaji wa Maendeleo ya Dunia ya kumkwamua kila mwananchi kuwa katika Maisha Bora kufikia 2030. 

“Malengo yetu makubwa ni kupambana na maadui watatu wa kitaifa akiwemo Ujinga, Maradhi na Umaskini lakini hasa ni kupigana na maradhi yanayosababishwa na Magonjwa ya Kuambukizwa ili kuboresha afya ya binandamu pamoja na mifugo. Hivyo tunatumia Teknolojia ya kisasa kuyabaini magonjwa hayo ili kuweza kupata suluhu na kuyaondoa na pia kukomboa watu pamoja na mifugo kutokana na magonjwa hayo”, amesema Prof. Misinzo.

Aidha Prof. Misinzo amesema wao kama watafiti Katika kuisaidia Jamii kuhakikisha inakuwa salama wameongeza wigo hivyo wanalenga na hata Magonjwa yanayoharibu Afya ya Jamii lengo likiwa ni kuyabaini Magonjwa hayo kabla hayajasambaa.

Kigoda cha Olive Tambo ni miongoni mwa Vigoda 10 barani Afrika na kimoja kati ya viwili vilivyopo nchini Tanzania. Vigoda hivyo vimeanzishwa kwa madhumuni ya kumpa heshima Oliver  Tambo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Afrika Kusini katika kutimiza miaka 100 tangu kuzaliwa kwake. 



















Post a Comment

0 Comments