SUAMEDIA

SUA kupitia Mradi wa YEESI Lab inatoa Mafunzo kwa Vijana kuhusiana na Mfumo wa Akili Bandia

 NA:Winfrida Nicolaus

Idara ya Uhandisi Kilimo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Mradi wa YEESI Lab inatoa Mafunzo kwa Vijana kuhusiana na Mfumo wa Akili Bandia ili kumsaidia Mkulima kuweza kugundua kwa haraka tatizo kwenye shamba lake bila kumtumia Afisa Ugani.

PICHA MAKTABA


Amebainisha hayo  Mkuu wa Mradi wa YEESI Lab na Mhadhiri kutoka SUA Idara ya Uhandisi Kilimo Dr. Kadeghe Fue wakati akizungumza mubashara kupitia SUA FM kwenye Maonesho ya 29 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Tanzania katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoani Morogoro.

Amesema YEESI Lab ni Mradi wa Mafunzo kwa vijana ambao unawawezesha kutengeneza  mifumo inayoweza kugundua aina za Mimea, Magugu, Magonjwa na Wadudu waharibifu kwa kutumia picha za Kamera ya kawaida au Simu ambayo wameita mfumo wa Akili Bandia.

Dr. Fue amesema Mradi huo utaunda mifumo katika Utambuzi na Uainishaji wa Magonjwa, Magugu, Wadudu waharibifu pamoja na makadirio ya Miche iliyoota shambani na Utabiri wa Mavuno na vyote hivyo vitafanywa kwa kutumia Picha za Kamera ya kawaida au Simu Janja.

 “Mradi wa YEESI Lab unalenga zaidi katika kuongeza uelewa kwa vijana wa Morogoro na Mikoa ya Jirani ili kukabiliana na matatizo mashambani kwa kutumia Simu Janja au picha za kamera ya kawaida ndio maana tumeita Mfumo wa Akili Bandia ambapo itamfanya Mkulima aweze kugundua kwa haraka tatizo kwenye shamba lake bila kumtumia Afisa Ugani”, amesema Dr. Fue

Ameongeza kuwa ukiachana na Mradi wa YEESI Lab kuna Mradi mwingine wa EPA Lab ambao ni Mradi Mama wenye lengo la kuvitumia Vifaa vya Kielectoniki kwaajili ya Kilimo Bora na cha Uhakika ili kuongeza Tija kwenye mazao.

Amesema Mradi huo unafanya kazi kama Maabara ya kutengenezea vifaa vya Kielectroniki vile vile utaenda kuwasaidia Wakulima katika shughuli zao za shambani ikiwemo kutambua maeneo yaliyopata shida kwenye shamba lake kwa kutumia vifaa hivyo vya Kielectroniki.




 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments