Na: Editha Mloli
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo SUA Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Joseph Sinde Warioba amelitaka Baraza jipya
la Tathlitha ya 13 la Chuo kufanya Tafiti juu ya suala la Chakula hususani
mafuta ili kuja na matokeo yanayoweza kuleta tija katika jamii kwa kuwa chuo
hicho kinafanya vizuri katika masuala ya tafiti ndani na nje ya nchi.
Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu huyo ametoa
agizo hilo leo Agosti 19, 2022 katika Hafla ya kushukuru Baraza la Tathlitha ya 12 liliomaliza muda wake na kuzindua Baraza
jipya la Tathlitha ya 13 iliyofanyika katika Ukumbi wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza ICE chuoni hapo.
Akizungumzia kuhusu utendaji kazi wa
Tathlitha ya 12 ambayo imehudumu kwa muda wa miaka mitatu tangu mwaka 2019
ambapo ndipo ugonjwa wa UVIKO -19 uliingia nchini Mkuu huyo wa Chuo amesema analipongeza
bazara hilo kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kuongoza na kusaidia kuendesha
vizuri masomo kwa wanafunzi wa chuo hicho.
Jaji Warioba amesema japo kuna changamoto
nyingi baraza jipya linapaswa kusaidia
katika kubana matumizi ya fedha zilizopo kwa kujifunza kutumia kile kidogo
kilichopo kwa ufanisi mkubwa ili kusonga mbele na kufikia malengo ya chuo.
Awali akizungumza mbele ya Mkuu wa Chuo,
Makamu Mkuu wa Chuo cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda hakusita
kutoa pongezi kwa Baraza la Tathlitha ya 12 kwa kazi kubwa waliyoifanya katika
kipindi hicho cha miaka 3 tangu Julai 1, 2019 hadi June 30, 2022.
Prof. Chibunda ametaja baadhi ya
mafanikio yaliyopatikana katika Baraza la Tathlitha ya 12 ikiwa ni pamoja na
mikutano ya kuidhinishwa kwa muundo mpya wa chuo pamoja na upanuzi wa shughuli
za chuo kama kuongeza Kampasi ya mkoani Katavi (Kampasi ya Mizengo Pinda), Tunduru
Pamoja na Shamba la mfano la Kampasi ya Edward Moringe.
Prof. Chibunda ameongeza kuwa mafanikio
mengine yaliyopatikana katika baraza hilo ni pamoja na chuo kutoa watafiti bora
nchini ambapo mara mbili mfululizo Chuo kimetoa Mtafiti namba moja ambaye ni
Prof. Ludovic Kazwala.
Hafla hiyo imehudhuriwa na watu
mbalimbali akiwemo Mkuu wa Chuo cha SUA, Makamu Wakuu wa Chuo, Wajumbe wa Baraza
la Tathlitha ya 12 na 13, Wakuu wa Ndaki mbalimbali, Wakuu wa Idara na Vitengo
mbalimbali.
0 Comments