SUAMEDIA

Waziri Mchengerwa aelekeza Afisa Manunuzi Mkuu Tarura kuondolewa ili kupisha Uchunguzi wa Ubadhirifu wa Fedha za Miradi

 Na. James K. Mwanamyoto-Kagera


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu-UTUMISHI, kumuondoa kwenye nafasi yake Afisa Manunuzi Mkuu wa TARURA ili kupisha uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha za miradi.

Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo hayo mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.

Mhe. Mchengerwa amesema, uamuzi wa kumuondoa mtumishi huyo, unatokana na taarifa za uwepo wa mikataba mingi iliyosainiwa na baada ya muda ikafanyiwa mapitio na kuongezwa fedha jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.

“Wakati uchunguzi unaendelea, Afisa Manunuzi Mkuu huyo aripoti Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora siku ya Jumatatu tarehe 20 Desemba, 2021 na apelekwe Afisa mwingine atakayetekeleza majukumu yake,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Aidha, amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kupitia mikataba yote ya TARURA na kuchukua hatua stahiki pale itakapothibitika kuna ubadhirifu wa fedha.

“Namuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwenda TARURA kupitia mikataba yote kwa makini ili achukue hatua stahiki kwa watendaji ambao wanashiriki vitendo vya ubadhirifu vinavyokwamisha taifa kusonga mbele,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amesema kama taifa, ni lazima kufanya maamuzi magumu pale inapobidi ili nchi iweze kupiga hatua katika maendeleo na wananchi wanufaike.

Amesema, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alipofungua fursa za kiuchumi katika utekelezaji wa miradi ya serikali, alitaka taifa lipige hatua katika maendeleo na sio watu wafanye ubadhirifu wa fedha za umma, hivyo tumuunge mkono kwa kupinga vitendo vinavyorudisha nyuma maendeleo.

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, Watumishi wa Umma hawana sababu ya kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ubadhirifu kwasababu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anajali maslahi yao na yeye ni msikivu kwa watumishi.

Mhe. Mchengerwa amefanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Kagera ambapo amezungumzat na watumishi, walengwa wa TASAF na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


James K. Mwanamyoto

Afisa Habari

Ofisi ya Rais-UTUMISHI

KAGERA










Post a Comment

0 Comments