- Roncliffe Odit
- BBC Swahili, Nairobi
Mojawapo ya matukio maarufu ya biashara mwaka huu ni sarafu za kutumiwa mtandaoni au cryptocurrency, ambayo ni sarafu ya kidijitali inayoweza kutumika kununua bidhaa na huduma.
Hata hivyo katika nchi nyingi za Afrika, mengi hayajulikani kuhusu sarafu za kidijitali. Lakini cryptocurrency ni nini na inafanyaje kazi?
Tuanze na sarafu za kawaida ambazo tumezoea kutumia. Ni shilingi, ni Dirham, ni Kwacha ama hata Dola.
Kote duniani, watu wanatumia pesa, iwe sarafu au noti kulipia bidhaa na huduma. Lakini sasa kuna mfumuko wa aina mpya ya sarafu. Sarafu za mtandao au sarafu za kidijitali. Kwa Kiingereza wanaziita blockchain ama cryptocurrency.
Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la Benki Kuu ya Tanzania jijini Mwanza, aliitaka Tanzania kujiandaa na matumizi ya sarafu za mtandaoni au Cryptocurrency.
'Najua bado nchi nyingi, ikiwemo Tanzania, hazijakubali au kuanza kuzitumia sarafu hizo. Hata hivyo wito wangu kwa Benki Kuu ni vyema muanze kufanyia kazi maendeleo hayo. Kujitayarisha tu, kuwa tayari,' alisema Rais Samia
Lakini turudi nyuma kidogo, ilikuwa mwaka 2008 wakati ambapo kulikuwa na mporomoko m'baya zaidi wa kiuchumi kote duniani. Mwanauchumi Satoshi Nakamoto, akaandika waraka wake kwa anwani 'Bitcoin - peer to peer - Electronic Cash System' akiutambulisha mfumo mpya wa fedha unaohusisha mtu kwa mtu, ama taasisi kwa taasisi bila mhusika wa kati.
Mtaalam wa cryptocurrency Mhandisi Balete Kabenda kutoka Tanzania anasema hii ilifungua ukurasa mpya.
'Unapokuwa unatuma fedha kutoka kwa mtu A hadi mtu B, ama kutoka kwa Benki A hadi Benki B, lazima ziende kwa Benki Kuu. Au kama ni mobile money, lazima zipitie kwa wale ambao wamewapa huduma.
Lakini teknolojia ya blockchain inahakikisha fedha zinatoka kwa mtu mmoja hadi mwingine bila kupitia mtu kati, ambaye hufanya gharama kuwa juu zaidi,' anaeleza Kabenda.
Na sawia Mhandisi Balete Kabenda -mtaalamu wa Cryptocurrency Tanzania na aina nyingine yoyote ya biashara, matumizi ya sarafu mtandao yamepata umaarufu mkubwa kote duniani.
Kabenda anasema kufikia sasa sekta hii ya sarafu ya mtandao ina utajiri wa zaidi ya Dola Trilioni 3 za Marekani, ikilinganishwa na Dola Trilioni 7 za Marekani ambazo zipo katika sekta ya Benki. Na hii ni licha ya kwamba sekta ya Crypto imekuwa ikitumika kwa angalau miaka 10 pekee.
Na zaidi ya miaka 10 tangu kuanza kutumika kwa sarafu za mtandao, mapinduzi makubwa ya mfumo wa kifedha yamefanyika. Sasa kuna Meme Coins,, au sarafu za mtandao ambazo ni za mzaha tu na bado watu wanakula faida. Mifano ya Meme Coins ni pamoja na Dogecoin, Shiba In na Hokk.
'Unaona picha mtandaoni, na mtu anaweka maneno na mara moja inakuwa maarufu. Hiyo ndio meme. Sarafu za meme ni sarafu za mtandao ambazo zinapata umaarufu mkubwa kwa kuhusishwa na meme au mizaha ya mitandaoni. Na kwa sababu ya umaarufu wa mizaha hiyo, watu wengi zaidi wanataka kuhusishwa na sarafu hizi.'
Mark Basa, mkuu wa shirika la Hokk Finance ambalo linataka kuzama zaidi katika sarafu za kidijitali barani Afrika, anasema Afrika imebaki nyuma kuhusiana na sarafu za kidijitali. Lakini wakati umewadia kubadilisha mtazamo, na kama si sasa, ni sasa hivi.
'Miaka tano ama kumi ijayo inategemea sana mikakati ya serikali. Kwa hiyo serikali ambazo zitaweka sera za sarafu za dijitali zitapata watu wengi wakiwa tayari kufanya kazi nao na pia sarafu hizo za mtandao,' anasisitiza Basa.
Na barani Afrika watumizi wa sarafu za mtandao wanasema wamepata faida kubwa.
Mmoja wao ni Peter Oduba kutoka Kenya.
'Nilinunua Dogecoin mwaka 2017. Sasa hivi majuzi, bilionea Elon Musk akawekeza Dola bilioni moja kwenye sarafu hizo. Na hapo nikauza zangu kidogo na kupata faida kubwa, mpaka nikanunua nyumba ya $100,000.'
Lakini sawia na biashara nyingine yoyote, ununuzi na uuzaji wa sarafu za mtandao una hasara zake.
Mark Basa ambaye amekuwa akifanya biashara ya sarafu za mtandao kwa miaka kadhaa anasema ili kuepuka kutapeliwa, kwanza fanya utafiti.
'Crypto ni soko kubwa sana, na kutakuwa na watu kadhaa wabaya, lakini pia kuna watu wazuri. Inabidi tu uwe makini, fanya utafiti, tumia muda, tumia siku kadhaa, au hata wiki kadhaa, uliza maswali kuhusu jinsi unavyohisi,' anasema Basa.
Kauli yake inaungwa mkono na Mhandisi Balete Kabenda kutoka Tanzania, ambaye anasistiza kwamba lazima serikali ziweke mikakati na sera muafaka ili kuwalinda raia.
'Kuwa na sheria na sera za utumizi wa sarafu mtandao inawezekana. Nchi nyingi tayari zimeanza kufanya hivyo. Hata Afrika Kusini tayari wana mswada katika bunge lao ili kutunga sheria kuhusu matumizi ya sarafu hizi. Kila kitu kinawezekana.'
Wadadisi wanasema muda umefika kwa serikali moja moja kuweka sera muafaka za kuruhusu raia kufanya biashara kwa kutumia sarafu za dijitali. Lakini kabla muda huo kufika, wananchi wasomi na wabunifu wanaendelea kuwekeza na kutumia cryptocurrency kote duniani.
CHANZO BBC
- Roncliffe Odit
- BBC Swahili, Nairobi
0 Comments