SUAMEDIA

Prof. Ludovick Kazwala : Nitaboresha michezo ya Majalisi kwa mwaka ujao wa 2021

 

NA. AYOUB MWIGUNE

Rais wa Majalisi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Ludovick Kazwala ameahidi kuboresha  michezo ya Majalisi kwa mwaka ujao wa 2021 ili ushiriki uwe mkubwa zaidi



Prof. Kazwala ameyasema hayo wakati akifunga michezo  ya Majalisi na kutoa zawadi kwa washindi walioshiriki kwenye michezo hiyo iliyofanyika siku ya Jumatano Disemba 2020 kwenye viwanja vya Kampasi ya Edward Moringe Sokoine zamani ikijulikana kama Kampasi Kuu SUA

.

“Kuna baadhi ya michezo haikuchezwa mwaka huu kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu, lakini mwakani tutajiandaa mapema na kuongeza michezo mingi zaidi na tutahakikisha ushiriki unakuwa mpana zaidi” amesema Prof. Kazwala

 

ProfKazwala amesema kuwa lengo la michezo ya Majalisi ni kuwakutanisha pamoja wahitimu na  wafanyakazi  wa SUA na kuwajengea mahusiano mazuri kupitia michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, pete, kikapu, kuvuta kamba, riadha, drafti, kurusha tufe na kucheza karata.

 

Naye mratibu wa michezo hiyo Dkt. Beda John Mwang’onde ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi kutoka SUA amesema kuwa michezo ya Majalisi hufanyika mara moja kila mwaka kwa ajili ya kuwakaribisha tena Chuoni wahitimu wa SUA

 

Dkt. Mwang’onda amewapongeza baadhi ya Majalisi na wafanyakazi wa SUA waliotoa muda wao kwa kushiriki kwenye michezo hiyo kwani michezo ni afya, michezo ni furaha na michezo ni burudani.

 

“Mwaka huu tumepata washiriki wazuri kama Prof.  Elliot Phiri ambaye kwa umri wake tusingetarajia kumuona akikimbia mbio za mita 100  na kushika nafasi ya pili hatukutegemea kabisa awashinde vijana kwenye mbio hizo” amesema Dkt. Mwango’mbe.

 

Akitoa neno la shukrani Makamu wa Rais wa Majalisi Dkt. Raymond J. Salanga ambaye ni Mhadhiri kutoka SUA amewapongeza Majalisi, wafanyakazi na wanafunzi kwa kujitoa kushiriki kwenye michezo hiyo ya Majalisi pamoja na kuwa na majukumu mengine lakini waliona umuhimu wa kushiriki wenye michezo hiyo.

 

“Tunakubali kuwa mwaka huu wa 2020 hatukuwa vizuri kama mwaka jana tuombe radhi kwenye mapungufu  yaliyojitokeza ni sababu zilizo nje ya uwezo wetu lakini tunahaidi kujipanga vizuri mwaka 2021” amesema Dkt. Salanga.

 

Bonanza la Majalisi SUA ni jumuiko kuu la wahitimu wote wa SUA ambalo hufanyika mara moja kwa mwaka, siku chache kabla ya kutunuku shahada kwa wahitimu wa Shahada za Awali, Uzamili na Uzamivu

 

Post a Comment

0 Comments