Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Mradi wa Chakula na Kilimo Asilia
na Lishe Anuwai unaojulikana kwa jina la FOOD and Local, Agricultural, and
Nutritional Diversity (FOODLAND) kimekusudia kuboresha lishe za watu wa
rika mbalimbali sanjari na kuleta tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti,
Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron Karimuribo wakati
akifungua mkutano wa uzinduzi wa Mradi huo Novemba 19, 2020 mjini Morogoro.
Prof. Karimuribo amesema Mradi huo wa FOODLAND utasaidia kuinua uchumi wa
kati na kwamba wanategemea tafiti zinazofanywa na SUA zitasaidia kuongeza
uzalishaji hasa katika kipindi hiki ambapo malighafi zinahitajika katika
kuendeleza viwanda vilivyopo nchini.
"Katika kuinua Uchumi wa Kati tunategemea kuongeza tafiti na tafiti
hizo tunatamani zisiishie kwenye machapisho bali ziwafikie wanajamii na taifa
kwa ujumla ili ziweze kuwa na matokeo makubwa katika kubadilisha maisha ya
watanzania", alisema Prof. Karimuribo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mratibu wa Mradi huo kwa upande wa Tanzania
Prof. Susan Msolla amesema lengo lao kubwa ni kuboresha lishe ya watanzania
pamoja na kutoa elimu itakayowawezesha watanzania kutumia vyakula vya aina
mbalimbali kwa lengo la kujenga afya zao.
"Nia kubwa ya Mradi huu ni kuboresha lishe ya watu, tunategemea
kupitia mradi huu tutatoa elimu na kupata takwimu za jinsi watu wanavyozalisha,
pia tunataka kujua sababu ni kwa nini watu wanashindwa kula vyakula vya aina
nyingi", amesema Prof. Msolla.
Kwa upande wake Kaimu Rasi wa Ndaki ya Kilimo Dkt. Rashid Suleiman amesema
mradi huo umekuja wakati muafaka kwani tafiti zitakazofanyika zitakisaidia chuo
cha SUA na Taifa kwa ujumla katika kuongeza uzalishaji wa chakula.
Awali akitoa akitoa maelezo kuhusu Mradi wa FOODLAND, Mkurugenzi wa Taasisi ya elimu ya
Kujiendeleza (ICE) ambaye pia ni mshiriki wa Mradi huo Prof. Dismas Mwaseba
amesema mradi huo unatekelezwa katika nchi mbalimbali duniani
Amesema "kuna taasisi mbalimbali duniani zinazoshiriki katika mradi
huu zikiwemo nchi sita za Afrika na nyingine za Ulaya, kwa Afrika mradi
unatekelezwa katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Tunisia na
Morocco".
Mradi wa FOODLAND ambao umezinduliwa leo umeanza rasmi mwezi Septemba mwaka
huu na utafikia kilele mwezi Agosti mwaka 2024.
0 Comments