SUAMEDIA

SUA mshindi wa tatu kwenye hesabu zilizoandaliwa kwa Ubora

Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimefanikiwa kushika nafasi ya tatu katika Mashindano yanayoandaliwa Mara moja kila mwaka na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu Kitaifa.





Akizungumza baada ya kukabidhi Tuzo ya kuwa mshindi wa tatu kwa Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda mnamo tarehe 11 Disemba 2019 ofisini kwake, Kaimu Afisa Mkuu fedha SUA Peter Willison amesema kuwa Bodi ya Kitaifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu kila mwaka inaalika Taasisi binafsi pamoja na Mashirika ya Umma kuingia kwenye shindano la kuona hesabu  zilizoandaliwa kwa Ubora wa Viwango vya  Kimataifa.
“Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa Chuo chetu kushiriki kwenye mashindano haya na kufanikiwa kuwa mshindi wa tatu katika kundi la Taasisi za Umma kwa  Elimu ya Juu" amesema Bw. Willison.
Ameeleza kuwa Bodi ya Uhasibu ilikuwa inaangalia kama Taasisi zote zilizoshiriki zimefanikiwa kupata zaidi ya asilimia 75 ya maksi walizoziweka na wengine waliokuwa chini ya maksi hawakuweza kuendelea kushindana. Katika tuzo hizo mshindi wa kwanza alikuwa Chuo cha Ustawi wa Jamii, wa pili alikuwa Chuo cha Mzumbe na mshindi wa tatu ni Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

Vile vile Kaimu Afisa Mkuu fedha SUA amekihakikishia Chuo mwaka ujao 2020 kufanya vizuri zaidi kwa kuyapitia na kuyarekebisha yale yaliyowafanya washike nafasi ya tatu mwaka 2019.
Kwa upande wa Makamu mkuu wa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael T. Chibunda amefurahishwa na mafanikio hayo huku akihitaji mafanikio makubwa zaidi kwa mashindano  yajayo.
       

Post a Comment

0 Comments