Na: Catherine M. Ogessa
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekipatia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA jumla ya shilingi milioni 750 ili kiweze kufanya ukarabati wa karakana mbalimbali za uhandisi Kilimo, yote hayo ni katika kutambua kuwa, chuo hicho kina sehemu kubwa katika azma ya kuleta mapinduzi ya Kilimo.
Akifungu kumbukizi ya 16 ya kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine inayofanyika SUA, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. LEONARD AKWILAPO amesema kuwa pesa hizo ambazo ni kupitia mradi wa kukuza ujuzi na stadi za kazi zinatolewa kwa SUA ili karakana ziwe bora na ziendane na mwenye jina la Chuo Hayati Sokoine
Amesema kuwa kama nchi wanatekeleza kwa vitendo maono ya hayati Edward Moringe Sokoine ambaye aliongoza nchi hii kwa moyo wa uwajibikaji, kufuata sheria na hali ya kujitoa na pia alikuwa miongoni mwa wazalendo wakubwa waliowahi kuwepo nchini.
“Mtu mwenye tabia njema na kiongozi aliyejitoa muda mwingi kwa ajili ya maendeleo ya watu wake na nchi kwa ujumla…., katika kuadhimisha kifo chake, tuna kila sababu ya kutafakari mawazo yake ambayo yalichangia katika kujenga msingi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi nchini”. Alisema Dkt. LEONARD AKWILAPO
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda amesema Chuo cha SUA katika kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine kimekuwa na kumbukizi tangu mwaka 1992 lengo likuwa ni kuyakumbuka mambo mazuri aliyoyafanya kwa maendeleo ya Tanzania, na kuyafanya maono yake kuwa hai kwaajili ya maendeleo ya taifa.
Miongoni mwa mambo ambayo wamekuwa wakiyafanya ni kuwa na mihadhara kutoka viongozi wa juu wa kitaifa, mihadhara ambayo imekuwa ikiakisi mambo ambayo Sokoine aliyafanya pamoja na maono yake katika maendeleo ya taifa.
“Kumbukizi ya mwaka huu inafanyika kwa namna tofauti ukilinganisha na zile za miaka iliyopita ……., Aidha chuo kimeandaa shughuli za maonesho za kazi za SUA pamoja na teknolojia zilizozalishwa chuoni hapa, kongamano la kisayansi pamoja na mdahalo wa kitaifa kuhusu kumbukizi ya hayati Ewdward Moringe Sokoine”. Alisema Prof. Chibunda.
Akielezea kuhusu uhusiano wa jina la SUA kuitwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Chibunda amesema kuwa tarehe 11 April, mwaka 1984, Hayati Edward Moringe Sokoine alihutubia kikao cha Bunge mjini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine bunge lilipitisha muswada na kuwa sheria ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Morogoro cha Kilimo.
Ameongeza kuwa wakati akitokea Dodoma April 12, 1984 alipata ajali mkoani Morogoro eneo la Wami Dakawa na kufariki ndipo baadae uongozi mpya wa chuo kikuu cha Morogoro kiliomba Serikali kuridhia mabadiliko ya jina la chuo kipewe jina la Sokoine kama njia mojawapo za kumuenzi kwa jitihada alizokuwa akizifanya.
Aidha Serikali iliridhia ombi hilo na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kikazaliwa na kuanza rasmi mwezi Agosti 1984 na hii ni kutoka na ushiriki wake wa kiwango cha juu katika maendeleo ya taifa kupitia Nyanja ya kilimo.
Akielezea kuhusu uhusiano wa jina la SUA kuitwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Chibunda amesema kuwa tarehe 11 April, mwaka 1984, Hayati Edward Moringe Sokoine alihutubia kikao cha Bunge mjini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine bunge lilipitisha muswada na kuwa sheria ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Morogoro cha Kilimo.
0 Comments