SUAMEDIA

Watafiti SUA na TPHPA wapata suluhisho la Viwavijeshi Vamizi nchini.

 Na: Calvin Gwabara – Tanga.

Wakulima wa zao la Mahindi walioshiriki kwenye Utafiti wa jaribio la kuangalia matumizi ya wadudu rafiki katika kupambana na viwavijeshi vamizi nchini wamefurahishwa na namna wadudu hao walivyoweza kuwatokomeza viwavijeshi na kuahidi kuachana na matumizi ya viuatilifu sumu endapo wadudu hao watapatikana kwa urahisi madukani.

Mtafiti Mkuu Prof. Gration Rwegasira akiwa kwenye moja ya shamba la Mkulima wilayani Kilosa

Wakizungumza na Waandishi wa habari Wakulima hao wamepongeza utafiti huo mzuri uliofanywa na Watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushiriakana na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) katika Mikoa ya Morogoro na Tanga  kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).

Akieleza kuhusu kile alichokiona Mkulima Salehe Alfan Ally Mkazi wa Dumila Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro amesema kuwa wakati watafiti hao wanaleta wadudu hao wadogo na kuwaweka shambani kwake hakuamini kama wanaweza kutokomeza kizazi cha viwavijeshi vamizi ambao wamekuwa wakiwakosesha mavuno pamoja na gharama kubwa wanazozitumia kununua viuatilifu sumu vya kuwaua pasipo mafanikio.

Mkulima Salehe Alfan Ally Mkazi wa Dumila Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro akionesha sehemu ya Mahindi yake yalivyobeba bila ktumia Dawa za wadudu.

Mimi walipowaweka wadudu hawa wakaniambia nisipulize dawa kabisa katika wiki ya kwanza mahindi yangu shambani yakadhoofika sana, nikawaza kupulizia dawa walipoondoka lakini nikasema ngoja nivumilie ila baada ya wiki moja iliyofuata mahindi yakaanza kubadirika na kuwa mazuri huku nikiendelea kuyapatia maji na mbolea na sasa angalia shamba zima hakuna mdudu, mahindi yamependeza na hakuna hata shina moja lililoshambuliwa, yaani viwavijeshi hakuna kabisa, haya ni maajabu kabisa” alieleza Salehe.

Amesema watu walipowaona watafiti shambani kwake wameondoka walimfuata kumuuliza, akawasilimulia kinachofanyika na hali ya mahindi yake yalipoharibika wakamcheka lakini baada ya muda nao hawakuamini wanachokiona huku wao mashamba yao pamoja na kupulizia dawa bado wadudu wanayashambulia huku wakiomba msaada nao kupata wadudu hao ili kuokoa mazao yao.

Nae Bw. Kasote Musa Kasote Mkulima wa mahindi kutoka Wilaya ya Muheza, Mkoani Tanga amesema Wadudu hao kwa jinsi walivyofanya kazi ni mkombozi kwa wakulima wa mahindi nchini ambao wamekuwa wakiachwa masikini baada ya mashamba yao kuvamiwa na Viwavijeshi vamizi tangu mwaka 2017 walipoanza kuwaona mashambani mwao.

 Bw. Kasote Musa Kasote Mkulima wa mahindi kutoka Wilaya ya Muheza, Mkoani Tanga akiongea na Waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu namna wadudu hao rafiki walivyofanya kazi.

Kwakweli sasa tunaona faida ya watafiti wetu na kwa jinsi wadudu hawa rafiki walivyofanyakazi shambani kwangu nikifika dukani nikakuta wadudu na dawa mimi moja kwa moja nitanunua wadudu hawa rafiki maana unawaweka kisha wanazaliana wao wenyewe na kuongezeka shambani lakini dawa lazima upige kila baada ya muda na ni ghali sana. Wengi hatuwezi, tunaomba sasa wapatikane madukani tuweze kuwanunua” alisema Bwana Kasote.

Aidha amesema shamba lake liligawanywa mara mbili na upande mmoja ukawekwa wadudu hao rafiki na mwingine haukuwekwa nikabaki napulizia dawa lakini upande ambao waliweka wadudu mazao yapo vizuri hayajashambuliwa wakati upande anaopuliza dawa mahindi bado yanashambuliwa.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo Mtafiti mkuu wa mradi kutoka SUA Prof. Gration Rwegasira amesema kwenye mashamba hayo waliweka wadudu aina mbili ambao ni aina ya Trichogramma mwanzae na Telenomous remus na matokeo ya maabara na kwenye kitalu nyumba yalionesha wanaweza kuwadhibiti viwavijeshi kwa asilimia zaidi ya 90. Vilevile katika  mashamba ya wakulima wamekuta udhibiti ni kwa zaidi ya asilimia 95 hadi 98.

Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kutoka (SUA) Prof. Gration Rwegasira akizungumzia matokeo ya utafiti huo na namna wadudu rafiki hao wanavyofanya kazi shambani.


Mtafiti huyo aliyebobea kwenye visumbufu vya mimea amesema uzuri wa wadudu hao wanashambulia mayai ya viwavijeshi vamizi kwa kuyatoboa na kutagia mayai yao humo na kwa kufanya hivyo kunasababisha Viwavijeshi Vamizi wasianguliwe bali wadudu rafiki. Hatimaye Viwavijeshi kutoweka shambani huku akisema muda mzuri kuweka wadudu hao ni mahindi yakishafikisha majani matatu hadi manne baada ya kupandwa hasa mkulima mayai ya Viwavijeshi yanapoanza kutagwa kwenye mahindi.

“Kwa hiyo sisi tunachofurahia ni kwamba mafanikio tuliyoona kwenye maabara na vitalu nyumba ya hao wadudu rafiki tumeyaona shambani vilevile. Mfano, mdudu rafiki aina ya Trichogramma mwanzae aliweza kushambulia asilimia mpaka 90% kwenye kitalu nyumba na hapa amepiga hizo na zaidi lakini yule wa pili aina ya Telenomous remus anakwenda hadi asilimia 98% yani karibia anaua kila kiwavijeshi na hii sasa inatudhihirishia kuwa wakulima wetu wanaweza kulima mahindi pasipo kupulizia sumu au viauatilifu vyenye viambata sumu kwenye mashamba yao na wakavuna vizuri” alifafanua Prof. Rwegasira.

Aidha akijibu maswali ya wakulima kuhusu ni lini wadudu hao rafiki watapatikana kwenye maduka ili waweze kuwanunua Mtafiti huo amesema baada ya kukamilisha majaribio hayo sasa wakwenda kufuata taratibu za kusajili wadudu hao kama kiuatilifu hai na baadae taratibu za kuwazalisha na kuwafanya wapatikane kwa wakulima nchi nzima utafanyika ili kuleta faraja kwa wakulima hasa wa mahindi ambao wamekuwa wakiteswa na viwavijeshi vamizi kwa miaka mingi.

Viwavijeshi Vamizi kutoka Amerika viliingia nchini mwaka 2017 kwenye mikoa michache lakini kufikia mwaka 2019 waliripotiwa kwenye mikoa yote ya Tanzania na kwa mujibu wa Shirika la umoja wa mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) Viwavijeshi Vamizi wanauwezo wa kushambulia mazao zaidi ya 80.

Post a Comment

0 Comments