Na: Calvin Gwabara - Dar es salaam
Wanafunzi
watatu wa shahada za juu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA)
wameiwakilisha vyema taasisi hiyo katika Mkutano wa Kimataifa wa ANH2025
Academy Week 2025 uliofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Mwanafunzi wa shahada ya Uzamivu Bw. Eward Mushi kutoka Idara ya Uchumi wa Kilimo na Biashara SUA akiwasilisha matokeo yake ya utafiti kwenye mkutano huo. |
Licha ya kuwa mwenyeji mwenza SUA iling’aa
kupitia ushiriki hai wanataaluma na Wanafunzi
wake watatu wa shahada za juu ambapo Wanafunzi wawili wa shahada ya uzamivu Bw.
Eward Mushi kutoka Idara ya Uchumi wa Kilimo na Biashara na Bi. Victoria
Kariathi kutoka Idara ya Lishe ya Binadamu na Sayansi ya Watumiaji waliwafanya
wasilisho la pamoja kwenye mkuatano huo (Learning Lab) kwa kushirikiana na
watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Tufts, Marekani.
Bw.
Mushi pia aliwasilisha utafiti wake kwa njia ya mawasilisho ya mdomo kuhusu "Vichocheo
vya Kimazingira vya Kiuchumi vinavyoathiri Matumizi ya Matunda na Mboga katika
Maeneo ya Vijijini na Mijini Tanzania," na alishiriki
kuendesha tukio maalum (Side Event) kwa kushirikiana na ANH Academy, ambapo
alitoa uzoefu wa mbinu bora za kufundisha na kujifunza uhusiano kati ya kilimo,
lishe na afya.
Kwa upande mwingine, Bi. Rosemary
Tegekanya, mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika ubora wa chakula na uhakika
wa usalama wake kutoka Idara ya Sayansi ya Chakula na Teknolojia, aliwasilisha
matokeo ya utafiti wake kuhusu "Tathmini ya Uelewa na Utendaji wa
Wakulima kuhusu Matumizi Salama ya Viwatilifu vya Organophosphate katika Mboga
Teuliwa kutoka Ilala, Dar es Salaam."
SUA imewapongeza wanafunzi hao kwa juhudi
zao za kushiriki katika mkutano huu maarufu wa kimataifa na kutoa wito kwa
wanafunzi wengine kuchangamkia fursa za kitaaluma katika majukwaa ya kimataifa
ili kuonyesha kazi zao na kupata uzoefu mpya.
Mkutano wa ANH
Academy Week unaendelea kuwa jukwaa muhimu la watafiti, wataalamu, na wadau
kujadili changamoto na suluhisho mbalimbali kuhusu kilimo, lishe, na afya
duniani.
Mwanafunzi wa shahada ya Uzamivu kutoka SUA, Bi. Victoria Kariathi kutoka Idara ya Lishe ya Binadamu na Sayansi ya Watumiaji akiwasilisha matokeo ya utafiti wake. |
0 Comments