Na: Calvin Gwabara – Dar es salaam.
Kamishna wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora nchini Dkt. Thomas Masanja apongeza kazi kubwa na
ngumu iliyofanywa na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) ya kukamilisha
zoezi la Urekebu wa Sheria Toleo la Mwaka 2023 na kumaliza kazi ya ufasili wa
sheria za nchi ili kuongeza uewelewa kwa jamii kuhusu sheria na mchakato mzima wa
uandishi wa sheria zinazowaongoza.
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Dkt. Thomas Masanja akizungumza mara baada ya kupata maelezo na elimu kutoka kwa wafanyakazi wa ofisi ya CPD. |
Pongezi hizo amezitoa
alipotembelea Banda la OCPD katika Uwanja wa Maonesho ya Biashara wa Mwl. J.K
Nyerere (SabaSaba) Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam yaliyoanza juni 18 na
kutarajiwa kuhitimishwa mwezi julai 13 mwaka huu.
“Nitumie nafasi hii kuipongeza
sana Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini kwa kazi kubwa waliyoifanya na
wanayoendelea kuifanya katika kuhakikisha jamii na wadau wa sheria wanapata
sheria kwa urahisi na kwa lugha mama ya Kiswahili, hii ni hatua kubwa sana ya
kujipongeza kama nchi.” alisema Kamishna Dkt. Masanja.
Aliongeza, “Kama mtu anayejua
kuongea kiingereza tu anapata shida kwenye kuelewa sheria, hali itakuwaje kwa
yule anayejua kingereza cha kusalimia tu Goodmorning?, na hali itakuwaje
kwa yule ambaye hajui kabisa lugha ya kingereza? Hivyo, unaweza kuona umuhimu
wa Ofisi yenu na kazi mnazozifanya kwa taifa letu.”
Amesema kuwa, kazi za OCPD, hasa
ya ufasili wa sheria ni ngumu, ikizingatiwa kuwa Kiswahili kina misamiati michache
ukilinganisha na kingereza, hivyo, zoezi hilo kubwa pamoja na ugumu wake lakini
linakwenda kuwasaidia watanzania wa ngazi zote katika kusoma na kujua sheria
hizo kwa lugha inayozungumzwa na wananchi wengi.
“Niwapongeze sana kwa kuamua kushiriki
maonesho haya na kuelimisha Wananchi na wadau wa sheria kuhusu sheria za nchi na
namna zinavyopatikana sambamba na majukumu ya Ofisi hii mpya na muhimu iliyo
chini ya Ofisi ya Mwansheria Mkuu wa Serikali.” Alieleza Dkt. Masanja.
Amewataka wananchi na wadau wa
sheria nchini sambamba na wafanyabiashara kutembelea banda hilo ili kujifunza
mambo mengi yanayohusu uandishi wa sheria, Urekebu wa sheria na Ufasili wa
sheria za nchi.
Kwa upande wake Afisa Uchunguzi
Mwandamizi kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Pontian
Kitorobondo amepongeza kukamilika kwa zoezi la urekebu wa sheria kwani wadau
wamekuwa wakipata tabu katika kutumia sheria na wakati mwingine kujikuta
wanatumia sheria ambazo sio sahihi kufanyia maamuzi bila kujua kuwa sheria
husika imeshafanyiwa marekebisho.
“Kupata toleo hili la Urekebu wa Sheria
la Mwaka 2023 kunakwenda kurahisisha sana matumizi ya sheria na utoaji wa haki
kwa jamii, na kuwafanya wadau kuacha kutumia sheria mbazo hazijahuishwa, hivyo
kuleta changamoto kwa watumiaji katika kupata haki na kutimiza wajibu wao
ipasavyo.
Ametumia nafasi hiyo pia kuiomba OCPD
kuona namna itakavyoweza kuwaelimisha wadau wa sheria nchini hususani taasisi
za Serikali kuhusu zoezi hilo la urekebu na kazi kubwa wanazozifanya katika Ofisi
hiyo ili waweze kupata msaada pindi wanapopata changamoto yoyote katika
matumizi ya sheria husika zozote.
Kwa upande wa raia kutoka Dar es
Salaam, Bwana Wile Kaale, amesema amepata elimu ya kina kuhusu mchato wa uandishi
wa sheria nchini tofauti na awali ambapo alikuwa anajiuliza inakuwaje wabunge
wanaweza kutunga sheria za nchi ilihali wengi wao hawana elimu ya sheria. .
“Binafsi nimefurahi sana
kutembelea banda la OCPD kwenye maonesho haya na kuweza kufahamu kuhusu uhusiano
wa majukumu baina ya Bunge na OCPD katika kutunga sheria katika kufanikisha
upatikanaji wa sheria bora za nchi yetu.” Alieleza Bwana Kaali.
Kauli
Mbiu ya maonesho ya 49 ya Kimataifa ya SabaSaba ni “Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar
es Salaam ‘Sabasaba’ – Fahari ya Tanzania.”
Mwandishi wa Sheria toka Ofisi ya Mwanishi Mkuu wa Sheria Bwana Philemon Mrosso akipokea pongezi OCPD kutoka kwa Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Dkt. Thomas Masanja. Bwana Philemon Mrosso akitoa maelezo kwa ujumbe kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini walipotembelea Banda la OCPD kwenye maonesho ya sabasaba jijini Dar es salaam. Bi. Happyphania Erick akitoa maelezo ya majukumu ya OCPD kwa Mkurugenzi msaidizi: Elimu kwa Umma na Mawasiliano wa Tume hiyo Bi. Zawadi Msalla alipotembelea banda ya OCPD. Bi. Happyphania Erick akimuelimisha bwana Wile Kaale aliyetembelea banda la OCPD kujifunza juu ya masuala ya utungaji wa sheria na nafasi ya ofisi hiyo katika zoezi hilo. Wakili wa Serikali bwana Vincent Masalu akimuonesha mwananchi aliyefika kwenye banda hilo Juzzuu za sheria zilizofanyiwa urekebu toleo la mwaka 2023. Kijana wa Skauti akisaini mara baada ya kutembelea banda la OCPD kwenye maonesho ya sababsaba jijini Dar es salaam. Wakili wa Serikali bwana Vincent Masalu akitoa maelezo kwa wananchi waliojitokeza kwenye banda la OCPD. Mwandishi wa Sheria toka ofisi ya CPD Bi. Mariam Possi akitoa maelezo kwa mwananchi kwenye banda la OCPD kwenye maonesho ya Kimataifa ya Biashara sabasaba jijini Dar es salaam. Bi. Happyphania Erick akimuonesha Afisa Uchunguzi Mwandamizi kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Pontian Kitorobondo baadhi ya kazi zilizofanywa na ofisi ya CPD.
0 Comments