SUAMEDIA

SUA na Benki ya Equity Tanzania kupanda hekta 100 za miti Madaba

Na: Gerald Lwomile

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  kwa kushirikiana na Benki ya Equity Tanzania inatarajia kupanda miti 100,000  katika eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 90 katika shamba la miti la SUA lililopo katika Kijiji cha Ifinga wilayani Madaba mkoani Songea.

Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyama Pori na Utalii Prof. Agnes Sirima (kushoto) akipanda mti na Mkuu wa Kitengo cha Uendelevu wa Benki ya Equity Tanzania Bi. Hellen Dalali

Akizungumza na SUA Media Juni 17, 2025 katika shamba la SUA, Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyama Pori na Utalii Prof. Agnes Sirima amesema zoezi hilo la upandaji miti lina manufaa makubwa kwa taifa kiuchumi, hifadhi ya mazingira na ajira.

Amesema Benki ya Equity Tanzania umekuja kuongezea nguvu na kasi katika upandaji wa miti kwani SUA wamekuwa wakipanda hekta 500 ambazo huingia zaidi ya miti 550,000 kwa mwaka.

“Ushirikiano huu umekuja kuongeza nguvu na kasi katika upandaji wa miti kwani SUA tumekuwa tukipanda hekta 500 kwa mwaka, kuanzia mwaka 2026 benki ya Equity Tanzania wamekuja kutuongezea nguvu” amesema Prof. Agnes Sirima.

Wafanyakazi wa SUA naEquity BenkiTanzania walioshiriki zoezi la uzinduzi wa upandaji miti wilayani Madaba

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uendelevu wa Benki ya Equity Tanzania Bi. Hellen Dalali amesema Benki ya Equity kupitia Idara yake ya Uendelevu ambayo pia ipo nchini wamekua wakisimamia sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchumi wa buluu, misitu, hewa ukaa, bioanuai na mazingira kwa ujumla.

“Tulijiwekea malengo kama Equity kupanda miti zaidi ya milioni 35 katika nchi zote tunazotoa huduma, kwa bahati mbaya kwa hapa Tanzania tulikuwa nyuma kidogo katika zoezi la upandaji miti lakini baada ya kuanzisha kitengo cha uendelevu tukaona tutafute wadau ambao watatusaidia kufikia lengo maana sisi hatuna utalaamu wa kupanda miti hivyo tunafuraha kushirikiana na SUA” amesema Bi. Hellen.

Awali akizungumza na ujumbe kutoka SUA Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Bw. Sajidu Idrisa Mohamed ameipongeza SUA kwa jitihada kubwa inayofanya katika kuhakikisha inaendeleza sekta ya misitu nchini.

Akizungumza katika kikao cha SUA na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mratibu wa Mahusiano baina ya sekta binafsi na chuo Dkt. Felix Nandonde amesema SUA itashirikiana na Benki ya Equity Tanzania kwenye zoezi la upandaji miti ikiwa ni moja ya maeneo ya mashirikiano na Benki hiyo kwa muda wamiaka mitano.








Post a Comment

0 Comments