Na Gerald Lwomile
Serikali imesema
itaendelea kupambana na udumavu unaoathiri zaidi ya asilimia 30 ya watoto chini
ya miaka mitano nchini, huku ikidhibiti tatizo la uzito kupita kiasi na
upungufu wa virutubishi kupitia Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Lishe wa
Sekta Mbalimbali.
![]() |
Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko akifungua mkutano |
Akifungua Wiki ya Mkutano
wa Kilimo, Lishe na Afya (ANH2025) Juni 23, 2025, Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, alisema kuna uhusiano
mkubwa kati ya kilimo na lishe. Amesisitiza kuwa kilimo chenye mwelekeo wa
lishe kinaweza kupunguza utapiamlo na magonjwa yatokanayo na lishe duni, huku
afya bora ikiongeza tija na kuimarisha maendeleo ya taifa.
“Tanzania, kilimo
kinachangia asilimia 29 ya Pato la Taifa na kuajiri zaidi ya asilimia 65 ya
wananchi. Ndiyo maana bajeti ya kilimo imeongezwa kwa asilimia 29. Serikali pia
inaendelea kutekeleza programu mbalimbali kama vile ‘Jenga Kesho Iliyo Bora’
(BBT), inayowasaidia wakulima wadogo kupata pembejeo bora, zana za kilimo,
miundombinu ya umwagiliaji na elimu ya ugani,” amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wa sekta ya
afya, Dkt. Biteko alisema maboresho makubwa yamefanyika, ikiwemo ongezeko la
asilimia 7 la vituo vya afya tangu 2021, ajira ya wahudumu wa afya ya jamii
wapatao 137,000, pamoja na kupanua huduma za kidijitali ili kupambana na
magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.
Awali, akimkaribisha Naibu
Waziri Mkuu kufungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Sayansi, aliyemwakilisha Waziri wa Sayansi na Elimu, alisema kupitia elimu bora
nchi inaweza kuongeza tija katika sekta za kilimo, afya na lishe.
Akizungumza katika
mkutano huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof.
Raphael Chibunda, alisema SUA inajivunia kuwa mwenyeji mwenza wa mkutano huo,
ambao unawaleta pamoja watafiti na watunga sera ili kuimarisha kilimo na lishe
nchini. “Lengo kuu la mkutano huu ni kuangalia namna ya kuboresha kilimo chetu
ili kitoe mazao yenye lishe bora, hivyo kupunguza magonjwa yanayosababishwa na
ukosefu wa lishe,” amesema Prof. Chibunda.
![]() |
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda akizungumza katika mkutano huo |
Naye Mwenyekiti wa
Mkutano huo, Prof. Sunnetha Kadiyala kutoka Shule ya Lishe na Tiba ya Magonjwa
ya Kitropiki ya London, alisema mkutano huu unalenga kuimarisha matumizi ya
tafiti na sayansi katika sera, kupanua wigo wa ushirikiano wa kimataifa, na
kuhakikisha vijana wanasayansi wanajengewa uwezo kupitia programu za mafunzo na
ushauri. Alisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utafiti wa kisayansi ili
kuboresha mifumo ya chakula, kupunguza njaa na kuhakikisha usalama wa chakula.
Tanzania imekuwa mwenyeji
wa Mkutano wa Kilimo, Lishe na Afya (ANH2025), ukijumuisha washiriki kutoka
zaidi ya nchi 50 duniani. Mkutano huu umeandaliwa na ANH Academy kwa
kushirikiana na Shule ya Lishe na Tiba ya Magonjwa ya Kitropiki ya London
(LSHTM) pamoja na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
0 Comments