SUAMEDIA

Kilimo cha Embe kumnufaisha Mkulima

 Na Editha Mloli

Ushauri umetolewa kwa wenye ardhi kutumia vema ardhi zao katika kilimo cha maembe ili kuweza kujikwamua kiuchumi kwa kuwa kilimo hiki kinalipa kama kitakuwa na matunzo mazuri pamoja na uzingatiaji wa namna ya kutunza zao hilo.



Wito huo umetolewa na Msimamizi wa Shamba la Mafunzo la Mfano kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Alpha Mtakwa wakati akizungumzia kuhusiana na ukuzaji wa zao la embe.

Mtakwa amesema kuwa kuna aina tofauti za maembe hapa nchini ambazo kama Mkulima ataamua kulima zao hili atajipatia fedha kila msimu kwa kuwa kila aina ya embe inaendana na msimu wake na hivyo anaweza kupata fedha mara dufu.

Ameongeza kuwa faida ya zao hili la embe likishashika ardhini haliwezi kufa hata kama sehemu hiyo ina ukavu kwa muda kwa kuwa mizizi ya embe ina nguvu japokuwa kuna wakati pia inaweza kukaa kwenye maji muda mrefu na bado likaendelea kuishi.

“Ni vema watu wenye ardhi zilizolala wakapanda maembe pamoja na kwamba maembe ni lazima ukapanda kwenye ardhi ambayo haituamishi maji lakini muembe una uvumilivu kwa kuwa unaweza ukakaa kwenye maji hata mwezi na usife na kama unaweza kuwa sehemu yenye ukame mkali unaweza kuvumilia pia usife”, amesema Mtakwa. 

Mtakwa pia amesema tofauti na kupanda maembe mashambani lakini pia ni vizuri ikapandwa majumbani pamoja na matunda mengine kutokana na pendekezo la Shirika la Chakula Duniani kwamba Tanzania haifikishi moja ya tatu ya ulaji wa matunda kwa hiyo ni vema kuzingatia ulaji wa matunda kwa ajili ya kuinua afya. 

Akizungumzia katika uzalishaji wa maembe nchini kwa miaka 10  iliyopita Tanzania ilikuwa nafasi ya 17 kwa nchi za Afrika katika uzalishaji wa maembe ambapo kwa sasa wamejitokeza watu wengi wenye uwezo wa kuzalisha zao hili na matokeo yake yanaonekana. 

Aidha ameendelea kuishauri jamii kuwa na vifaa vya kuhifadhia maembe kwa kipindi ambacho yanapatikana na baada ya hapo yakipotea inakuwa faida ya wale waliohifadhi kwa wao kuendelea kula matunda hayo au hata kutengenezea sharobati.

“Mimi ningeshauri hata watu binafsi waweze kuwa na vyumba vya baridi au vifaa vile vyenye uwezo wa kuhifadhi kitu kisiharibike wakanunua maembe kwa wingi wakahifadhi halafu kipindi ambacho hakuna maembe wakawa wanauza maembe yenyewe au ule uji uji wa embe kwa ajili ya kutengenezea sharobati”, amesema Msimamizi huyo wa Shamba la Mafunzo la Mfano kutoka SUA.

 


Post a Comment

0 Comments