Na: AYOUB MWIGUNE
Wanafunzi wa Shahada za kwanza, pili na tatu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wamepatiwa mafunzo yenye lengo la kutambua njia mbalimbali za kuandika maandiko ya kitafiti ambayo ndani yake yatawezesha kutambua mbinu za kuja na tafiti bunifu zenye kutatua changamto zinazoikabili jamii.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Utafiti na Machapisho kutoka Kurugenzi, ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Japhet Kashaigili wakati akifunga mafunzo kwa wanafunzi hao wa SUA.
Prof. Kashaigili amesema anaamini mafunzo hayo yamewajengea uwezo wanafunzi kutoka SUA katika kufanya tafiti bunifu ambazo zitaleta tija na mabadiliko katika Jamii, huku akiwaomba wanafunzi hao kutenga muda kwa ajili ya kuhakikisha kile walichojifunza katika semina hiyo wanakwenda kuwafundisha wanafunzi wengine.
“Chuo Kikuu cha Sokoine Kilimo SUA kitaendelea kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kuwa elimu mliyoipata mnaitumia ipasavyo katika kuleta mafanikio katika jamii ” alieleza Prof. Kashaigili.
Kwa upande wao washiriki katika mafunzo hayo Bi. Rehema Anthony , Bw. Mihonjo Titus pamoja na Bw. Paul Kisena wamewashukuru waandaji wa Mafunzo hayo huku wakieleza kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa katika kujenga uwezo wa kufanya tafiti mbalimbali zenye kuleta tija katika jamii.
Naye Mkufunzi katika mafunzo hayo ambaye pia ni Mtaalamu wa Hataza na Haki Miliki Ubunifu Dk. Georges Shemdoe amesema anategemea kuona Wanafunzi hao wakipiga hatua kutokana na Mafunzo hayo waliyopata kutoka kwa Wakufunzi mbalimbali .
KATIKA VIDEO
0 Comments