SUAMEDIA

Wakulima watumieni wawekezaji kuinua ujuzi na maarifa katika kilimo- Prof. Chibunda


Na Gerald Lwomile

Ilula, Iringa

Chuo Kikuucha Sokoine cha Kilimo SUA kimesema ili nchi ya Tanzania iendelee katika sekta ya kilimo juhudi za makusudi zinahitajika katika kuhakikisha wananchi wanachukua jukumu la kujiletea maendeleo kwa kubadilisha aina ya kilimo na kufanya kiwe cha kibiashara kwa kutumia mbinu bora za kilimo yaani kuzipokea na kuzitumia mbinu za wawekezaji  wenye nia ya kuikwamua jamii katika changamoto mbalimbali 


Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda (wa pili kushoto kwenye bango) Meneja wa Mradi wa “Farm For the Future” Bw. Osmund Ueland,(wa kwanza kushoto aliyeegemea bango), Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Taaluma Prof. Peter Gillah (watatu toka kulia walioshikilia bango)  pamoja na Viongozi wengine katika picha ya pamoja. 



Hayo yamesemwa February 18, 2020 Ilula mkoani Iringa na Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda wakati wa ziara ya siku moja ya kutembelea uwekezaji katika kilimo biashara unaofanywa na “Farm For the Future”

Prof. Chibunda ambaye katika ziara hiyo aliambatana na viongozi na wataalam mbalimbali kutoka SUA amesema wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kama watatumia mbinu bora za kilimo na kukubali kuasili mbinu zinazotumiwa na wawekezaji wakubwa wanaweza kuwa na uzalishaji wenye tija ambao utainua maisha yao na wataweza kujiletea maendeleo kwani wapo wawekezaji ambao wana nia ya dhati ya kutaka kusaidia jamii

“Shamba hili linatupa mfano mzuri kwamba watanzania wa kipato cha chini au kipato cha kati ni vizuri tukaweka mazingira mazuri ya kushirikiana na wawekezaji badala ya kugombana nao kwa sababu kuna mengi ya kujifunza kutoka kwao, mfano huyu hapa ameanza kuwafundisha wasichana wadogo  ambao wamepata mimba kabla ya kuolewa kulima maharage mabichi yanayosafirishwa kwenda nchi za ulaya…. Kwa hiyo nitoe wito kwa watanzania ni vizuri tunapopata wawekezaji wakweli na wasio matapeli basi tushirikiane nao ili kujiletea maendeleo”
Makamu huyo wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ameongeza kuwa SUA itaendelea na kazi ya kuhakikisha inawafikia wakulima katika maeneo yao kwani hivi sasa inaangalia uwezekano wa kushirikiana na mwekezaji huyo ili kutumia shamba hilo katika mafunzo na tafiti kwa wanafunzi wake na matokeo ya tafiti hizo yatanufaisha wakulima wote nchini kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa Rais Mhe. Dkt John Pombe Magufuli

Akizungumza na SUA Media Meneja wa Mradi huo wa “Farm For the Future” Bw. Osmund Ueland amesema wao pamoja na kuwa na nia ya dhati ya kufanya kilimo biashara lakini pia wamelenga kuhakikisha wanaisaidia jamii ya wana Ilula katika kutambua kuwa kilimo ni moja ya njia kubwa za kujipatia kipato
Amesema kuwa baada ya wao kupata shamba hilo waligundua kuwa kuna shida katika udongo wa eneo hilo na kuwa hauna rutuba ya kutosha hivyo kazi kubwa ilikuwa ni kuhakikisha wanarutubisha udongo huo kwa kutumia njia za kisasa ikiwa ni matumizi ya mbolea

“Na sasa tunataka pia kutumia njia ya umwagiliaji katika kilimo cha mahindi na macadamia ... Lakini pia ni muhimu kwetu kufanya kilimo cha kibiashara ili kuendelea kuisaidia jamii, tumekuwa na timu ya mafunzo ambapo tumekuwa tukifundisha wakulima wadogo, wanafunzi  na jamii kwa ujumla kufahamu kuwa kilimo ni muhimu kwa maisha yetu ya sasa na ya baadae”

Naye meneja wa shamba hilo Bi. Grace Kimonge amesema pamoja na kuendelea na kilimo biashara katika eneo hilo lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na hali ya hewa kwani mvua zimekuwa hazina uhakika lakini pia shamba lina mawe mengi jambo ambalo yanaathiri ufanisi wa kutumia trekta

Shamba laFarm For the Future lina jumla ya ekari 651 ambazo zina mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na mahindi, alizeti na hivi sasa wanajianda kulima macadamia zao ambalo linadaiwa kuwa na soko kubwa nje ya nchi.



Zaidi fuatitilia:-

www.ffftanzania.com

http://www.farmforthefuture.net/contact/

http://www.farmforthefuture.net/

VIDEO BOFYA HAPA CHINI

Post a Comment

0 Comments